April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Palestina yatoa msimamo UN

Spread the love

RAIS wa Palestina, Mahmoud Abbas amesema, kama Israel itaendelea kukwapua ardhi yake katika mji wa West Bank, itajiondoa kwenye mikataba yote iliyoingia na taifa hilo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).

“Wiki moja kabla ya uchaguzi wa Isreal hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu alitoa ahadi ya kupora maeneo ya Bonde la Yordani.

“Iwapo atachaguliwa kuendeleea kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, licha ya ukweli kwamba eneo la Bonde la Yordani yanamilikiwa na Palestina, Tunakataa na kulaani kabisa mpango huu haramu na unaokiuka sheria za kimataifa… Palestina itasimamisha mikataba yote iliyosainiwa baina yake na Isreal” amesema.

Rais Abbas ametoa kauli hiyo kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN), tarehe 27 Septemba 2019 wakati akitoa hotuba.

Kiongozi huyo wa Palestina ameeleza kushangazwa na hatua ya umoja huo kushindwa kutangazwa Uhuru wa Palestina kama ambavyo ilitarajiwa mwaka huu.

“Kwa masikitiko nasimama mbele ya kikao hiki kwa mara nyingine tena, nikibeba huzuni kubwa na uchungu ambao umevumiliwa kwa muda mrefu wa watu wangu. Licha ya yote, bado wana tumaini kubwa la kupata uhuru kama mataifa mengine yote ya ulimwenguni,” Rais Abbas amesema.

Kutokana na kuelemea upande mmoja katika utatuzi wa mgogoro kati ya taifa lake na Israel, Rais Abbas ameilani Marekani na kueleza kwamba, hakuna uwezekano wa taifa hilo kusimamia haki katika utatuzi wa kile kinachoendelea Mashariki ya Kati.

Kiongozi huyo amesema, Marekani imefanya mambo mengi yaliyo wazi na kwa kificho katika kuibeba Israel, ikiwa ni pamoja na kufunga ofisi za chama chake cha PLO mjini Washington. 

Pia taifa hilo limehamishia ubalozi wake mjini Jerusalem sambamba na kuzuia fedha zilizokuwa zikitolewa kama msaada kwa Shirika la Msaada na Kazi la UN kwa wakimbizi wa Palestina (UNRWA). 

“Hatua zote hizi zinaonesha upendeleo wa wazi,” amesema na kuongeza kwamba, licha ya Marekani kuja na mpango wa amani uliopewa jina la “Deal of the Centuary,” Palestina haitashiriki mazungumzo yoyote. 

Pia Rais Abbas amelaani hatua ya Israel kuendele kudhoofisha taifa lake kwa kushikilia mapato yake jambo lililosababisha kuyumba ikiwa ni pamoja na kushindwa kuhudumia wananchi wake.

Pia ameonesha imani yake kwa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, kamwe haiwezi kuvumilia ukatili wa Israel wa kuzuia mapato ya Wapalestina sambamba na mpango wa uporaji wa ardhi yake katika bonde la Jordan.

Rais Abbas amewaambia wajumbe wa UN kwamba, taifa lake linasimamia misingi ya demokrais kama ilivyo kwenye mataifa mengine duniani. 

Na hivyo, baada ya mkutano huo, pindi atakaporejea nyumbani (Palestina) atatangaza tarehe ya kufanya uchaguzi mkuu huku akitoa wito kwa UN na mashirika husika kufuatilia uchaguzi huu.

Katika salamu kwa raia wa taifa lake, Rais Abbas amewataka kuendelea kudumisha amani sambamba na kupigania haki na uhuru wao bila kuchoka.

error: Content is protected !!