Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mawakili wa Mbowe wambana shahidi
Habari za SiasaTangulizi

Mawakili wa Mbowe wambana shahidi

Spread the love

 

MAWAKILI wa utetezi, Jeremiah Mtobesya na John Mallya wamembana shahidi wa pili wa Jamhuri, Justin Elia Kaaya kuhusu maelezo aliyoyatoa kuhusu kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni leo Jumatano, tarehe 27 Oktoba 2021, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam.

Katika maelezo yake kulikuwa na tofauti ya mwaka ambapo shahidi alitaja mwaka 2018 wakati maelezo yanasema 2017 pamoja na jinsi walivyofanya kazi na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Aidha, kwenye maswali ya mawakili, kuna nyakati shahidi huyo alikuwa anataka kukaa kujibu hadi Jaji Joackim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo, kumtaka kufanya hivyo.

Pia, maelezo ambayo alihojiwa na mawakili hao, yamepokelewa kama kielelezo namba moja cha utetezi.

Fuatilia mahojiano yenyewe yalivyokuwa, baina ya mawakili hao kwa nyakati tofauti na Kaaya.

Jaji: Sasa tulikuwa tumebakisha upande wa cross-examination na ningependa kuanza na wakili wa mshitakiwa namba moja.

Mtobesya: Nitakuwa sahihi nikisema kwamba katika ushahidi wako hukutoa uthibitisho wako kwamba ulikuwa ukifanya kazi kwa Ole Sabaya?

Shahidi: Siyo sahihi.

Mtobesya: Mwambie sasa Mheshimiwa Jaji ni uthibitisho upi umetoa mbele ya mahakama hii.

Shahidi: Muulize Mheshimiwa Mbowe ndiyo atakwambia kama nilikuwa nafanya kazi.

Jaji: Mbowe siyo shahidi.

Jaji: Labda wakili urudie swali.

Mtobesya: Ni sahihi kuwa umesema ulikuwa unafanya kazi na Ole Sabaya?

Shahidi: Sahihi.

Mtobesya: Ni sahihi sasa kwamba hukutoa chochote mahakamani kuthibitisha?

Shahidi: Ndiyo. Sikutoa.

Mtobesya: Umesema katika ushahidi wako kuwa ulikuwa unasafikiri kutoka Longido kuja Moshi na kutoka Arusha kuja Moshi. Ulikuwa unatumia usafiri gani?

Shahidi: Usafiri wa umma.

Mtobesya: Ni matumaini yangu kuwa ukipanda basi la umma unapewa tiketi. Mwambie sasa Mheshimiwa Jaji kwamba wewe hukutoa tiketi.

Shahidi: Sikutoa tiketi kwa sababu nilipanda njiani.

Mtobesya: Kwa hiyo nipo sahihi kwamba hukusafiri kwa sababu hukutoa tiketi wala uthibitisho wako wowote hapa Mahakamani?

Shahidi: Siyo sahihi. Siyo lazima uwe na tiketi kuthibitisha.

Mtobesya: OK. Tunashukuru. Tangu ukutane na Mbowe mpaka unakutana na Inspector Swila ni muda umepita?

Shahidi: Umeuliza swali siyo sahihi.

Jaji: Uliza na mawakili wa Serikali. Wamenyamaza na Mahakama haijaingilia ujue hilo swali ni sahihi. Utatakiwa ujibu.

Shahidi: Jibu sifahamu.

Mtobesya: Tangu huyo unayemwita Mbowe mkutane ni muda gani umepita?

Shahidi: Mwaka moja na nusu.

Mtobesya: Kuna lolote alikuachia afande Swila baada ya kukuandika maelezo?

Shahidi: Hakuna aliloniachia baada ya kuandika maelezo. Alinipa vitu vyangu nikaondoka.

Mtobesya: Kwa hiyo Swila hakukuambia kwamba siku moja maelezo yako anayoandika yatatumika kama ushahidi?

Shahidi: Hakuniambia.

Mtobesya: Alichokiandika alikupa ukakisoma?

Shahidi: Ndiyo. Alinipa nikasoma.

Mtobesya: Ukajiridhisha kwamba ulichokisema ni sahihi?

Shahidi: Ni sahihi ndiyo.

Mtobesya: Hakuna wakati alikuambia kuwa umwambie kila kitu unakijua?

Shahidi: Hapana.

Mtobesya: Una uhakika ulichoandika ndicho ulichosema leo Mahakamani?

Shahidi: Ndiyo hicho hicho.

Mtobesya: Kwa Bahati nzuri sisi mawakili wa utetezi tuna nafasi ya kupewa nyaraka za maelezo mliyoandika.

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji naomba nipewe original document ya hii. Na msingi wangu wa kuomba ni kifungu cha 164 cha Sheria ya Ushahidi.

(Mawakili wa Serikali wanasema hawana pingamizi)

(Mtobesya anatembea kumfuata shahidi alipo)

Kimya kidogo kinatawala.

Shahidi: Haya ndiyo maelezo yangu ya kwanza.

Mtobesya: Unaweza kusoma?

Shahidi: Ndiyo.

Mtobesya: Soma tarehe kisha soma mtu aliyeandika ni nani.

Shahidi: Ndiyo haya.

Mtobesya: Naomba nikuulize kuhusu hii statement yako dhidi ya ulichokisema leo.

Mtobesya: Nilianza kutengeneza msingi kwa kuuliza, je, alichokisema hapa ndicho kilichopo kwenye statement? Sasa kama anataka twende hivyo tutaenda.

Jaji: Hapana.Tuwasaidie wateja wetu.

Wakili wa Serikali: Provisory mstari wa nne ndiyo inakataza.

Jaji: Tueleze nyie mmelewa nini?

Wakili wa Serikali Chavula: Maamuzi ya kifungu hiki yametolewa uamuzi na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Lilian Otesi Vs Jamuhuri, namba 77 katika rufaa ya Jinai ya 251 Mwaka 2008 katika Mahakama ya Rufaa. Katika kesi hii ukurasa wa 25 Mahakama ilisema yafuatayo:

“Kinachozungumzwa pale ni sawa na Kifungu namba 154 cha Sheria ya Ushahidi kama kilivyogawanyika maeneo mawili. Eneo la kwanza shahidi anaweza kudodoswa kupitia maelezo yake aliyoyaandika nyuma. Eneo la pili anaweza kuhojiwa kuhusu masuala yake hayo hayo bila kumwonyesha maelezo yake.

Wakili wa Serikali Chavula: Lakini kama inadhamiriwa kumpima mkanganyiko wake shahidi kuna utaratibu unaotakiwa kufuatwa. Na hivyo kabla ya kuthibitisha amwelekeze kwanza. Tofauti na yeye kaenda na kumfuata.

Mtobesya: Rafiki yangu anarejea vifungu viwili tofauti. Wakitaka hayo ningefika huko kwa sababu hata kesi ya Alberto Mendez imejadili hayo na mimi nilikuwa ni sehemu ya ile kesi. Kwa hiyo nafahamu ninachofanya.

Wakili wa Serikali: Kifungu cha 164 hakisimami peke yake. Kusimama kwake kunategemea kifungu cha 154. Na huo ndio msimamo wa Mahakama.

Mtobesya: Tusaidiane Mheshimiwa Jaji. Dhumuni la Kifungu cha 164 ni kumchanganya (contradict) shahidi. Mimi nilikuwa nimeanza kwenye kifungu cha 154. Sikuwa nimefika huko.

Jaji: Wao wanasema wana hukumu ambayo wanaweza za kutu- supply. Nafikiri ni vyema basi tuweze kuona tu.

Mtobesya: Hili suala linaweza kuibuka tena mbeleni. Tunaomba liwe cleared kabisa na Mahakama.

Wakili wa Serikali: Tunaomba dakika 15.

Jaji: Sawa. Tunaahirisha kwa dakika 15.

Kesi inatajwa tena. Ni kesi namba 16 ya mwaka 2021.

Jopo la mawakili wa Serikali wakiongozwa na Robert Kidando limetimia kama lilivyokuwa na anasema wapo tayari kupokea maelekezo ya Mahakama.

Jaji: Muda mfupi wakati wa dodoso na upande wa utetezi, upande wa utetezi waliomba Mahakama iruhusu itoe maelezo yaweze kutumika kwa nakala halisi P4. Baada ya mawakili wa utetezi kusimama, upande wa Serikali walisimama na kusema utaratibu haukufuatwa. Baada ya hapo pande zote walisema kuna maamuzi. Nikaomba maamuzi hayo.

1 Nyaraka inatakiwa itolewe. Hilo limeshafanyika.

2 .Nyaraka hiyo inapaswa isomwe katika maeneo anayotaka kumuuliza maswali ili kum- contradict.

Jaji: Mahakama hii inasema kwa kuwa huo ndio utaratibu basi unatakiwa ufuatwe na kuendelea na shughuli.

Wakili Mtobesya anarudi kwa shahidi na anaiomba Mahakama impatie tena nyaraka. Shahidi anaulizwa na anasema anaweza kuisoma.

Shahidi: Anaanza kuisoma.

Katika maelezo yake ansoma alishawahi kuwa msaidizi wa Katibu wa CCM Longido. Amesomea Hotel Management.

Alishawahi kufanya kazi na Sabaya kama msaidizi wake na aliacha kazi kwa Sabaya kwa sababu alitaka kurudi Longido na alienda kwa ajili ya kumfuata mchumba wake. Anarudia kuwa alipigiwa simu na Freeman Mbowe na kwamba alifuatwa Longido.

Shahidi (akisoma): “Freeman aliniambia kuwa nilitumiwa 50,000 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai Mama Helga na kumtomgoza.

Nilishangaa sana kwamba alijuaje kwa sababu ilikuwa ni kweli nilimtongoza. Alinipigia simu tukutane Moshi. Alinipigia niende Keys Hotel. Na siku nyingine tulienda Aishi Hotel.

Mtobesya: Soma eneo linalosema mimi nilikwenda kwa kutumia nauli yangu.

Shahidi: Mimi nilikwenda kwa kutumia nauli yangu, na nilipofika alikuja kunichukua.

Mtobesya: Ieleze Mahakama kwamba huyo mlinzi alikuwa diwani wa Kiboriloni.

Shahidi: Nilisema.

Mtobesya: Elezea sasa hapo katika maandishi yako humo kuna mlinzi anaitwa Bwire.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji mimi leo nilikuwa nafafanua.

Mtobesya: Hakuna mahala kwenye statement inaonyesha kuna mlinzi anaitwa Bwire.

Shahidi: Statement haionyeshi.

Mtobesya: Kwenye statement yako kuna sehemu inasema baada ya kukutana mara ya pili kwamba ulimtajia majina huyo Mbowe watu wanaotembea na Sabaya.

Shahidi: Majina hayajaandikwa hapa kwenye statement.

Mtosebya: Ulipokutana mara ya tatu ulisema ulimtajia pia najina. Hayo majina yapo kwenye maelezo yako?

Shahidi: Hayapo.

Mtobesya: Wakati unaongozwa na Wakili Wa Serikali na huyo uliyemuita Mbowe ulimpigia Sabaya na baadae Mbunge uliyemjulisha. Je, hayo yapo kwenye statement yako?

Shahidi: Hayapo.

Mtobesya: Pia wakati wakili wa Serikali anakuongoza nilisikia majina ya Hotel na clubs ulizotaja kwa majina yake. Hizo taarifa zipo humo kwenye statement yako?

Shahidi: Hazipo.

Mtobesya: Wakati Wakili wa Serikali anakuongoza huyo uliyesema Bwire alitamka kuwa Sabaya ni mtoto mdogo atamchezesha. Je yapo kwenye statement?

Shahidi: Hayapo.

Mtobesya: Wakati Wakili wa Serikali anakuongoza umesema wewe unajishughulisha na kilimo na ukasema unavyofanya kilimo. Je, yapo hapo kwenye statement?

Shahidi: Hayapo.

Mtobesya: Soma kwa Sauti kuanzia sehemu unayosema kuwa ulikuwa msaidizi wa Katibu wa CCM.

(Shahidi anasoma kuwa alikuwa msaidizi wa Katibu wa CCM na mwanaharakati wa CCM).

Mtobesya: Wakati Wakili wa Serikali anakuongoza ulisema kuwa wewe ulishawahi msaidizi wa CCM?

Shahidi: Hapana.

Mtobesya: Je, ungependa maelezo uliyoyaongea leo yaingie kwenye ushahidi wako?

Shahidi: Ndiyo kwa sababu nimeongea chini ya kiapo ningependa yaingie kama ushahidi.

Jaji: Upande wa Serikali?

Wakili wa Serikali: Hatuna pingamizi mheshimiwa.

Jaji anaandika wakati mahakama iko kimya na Wakili Mtosebya amekwenda kukaa kwenye nafasi yake.

Jaji: Kwa sababu imeombwa na shahidi kuwa maelezo hayo hayajapingwa na Mahakama, na haijapingwa na upande wa mashitaka, basi Mahakama imepokea maelezo hayo kama kielelezo namba 1.

Mtobesya: Naomba kuendelea Mheshimiwa Jaji.

Mtobesya: Nitakuwa sahihi nikisema kwa kipindi hicho mpaka unaandika statement ulikuwa unajishughulisha na siasa?

Shahidi: Siyo sahihi kwa sababu mimi ni mwandishi ninayepiga picha siyo mwanasiasa.

Mtobesya: Kwa hiyo wewe siyo mwanachama?

Shahidi: Siyo mwanachama wa chama chochote.

Mtobesya: Ni lini uliiacha kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi?

Shahidi: Sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote kile.

Mtobesya: Hujawahi kuwa karibu na viongozi wa kisiasa?

Shahidi: Nimesema kuwa nimekuwa karibu na viongozi wa Serikali na siasa.

Mtobesya: Unaweza kumtajia Mheshimiwa Jaji ni akina nani uliwahi kuwa nao karibu?

Shahidi: Mrisho Gambo, Daqaro na Sabaya.

Mtobesya: Hujawahi kuandika barua ukiwa gerezani kwa viongozi wa kisiasa wakusaidie kwenye kesi iliyokuweka jela?

Shahidi: Sijawahi.

Mtobesya: Hujawahi kutembelewa na viongozi wa kisiasa ukiwa gerezani?

Shahidi: Sijawahi.

Mtobesya: Ulikutana na mheshimiwa Mbowe gerezani tarehe ngapi?

Shahidi: Tarehe 26 Julai 2021.

Mtobesya: Maelezo yako umeandika lini?

Shahidi: Siku mbili baada ya kutoka gerezani.

Mtobesya: Na umesema wakati umefika Mahakamani Kisutu siku hiyo, mlielekezwa nini siku hiyo?

Shahidi: Baada ya upelelezi kukamilika tumeonekana hatuna hatia tena>

Mtobesya: Unakumbuka namba ya kesi ulikuwa umeshitakiwa nayo?

Shahidi: Sikumbuki.

Mtobesya: Naweza kusema Kesi namba 63 ya mwaka 2020.

Shahidi: Sahihi.

Mtobesya: Unakumbuka mashitaka uliyoshitakiwa nayo wewe binafsi?

Shahidi: Kushiriki vikao. Kula njama za kutenda vitendo vya ugaidi na utakatishaji.

Mtobesya: Kwa niaba ya mshitakiwa wa kwanza naomba tuishie hapa.

Mallya: Mheshimiwa Jaji naitwa John Mallya. Nina maswali machache (anamtazama shahidi na kumwambia) Jibu kwa sauti.

Mallya: Diwani analipwa shilingi ngapi?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Diwani analipwa posho shilingi ngapi?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Kwa ufahamu wako wewe Sabaya alikuwa anakulipa kutoka mfuko gani?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Kwa hiyo wewe hukutaka kabisa kujua kama anaiba au anatoa wapi?

Shahidi: Sikujua.

Mallya: Alikuwa anakulipa shilingi ngapi?

Shahidi: 300,000/-.

Mallya: Kwa picha au kwa mwezi?

Shahidi: Kwa mwezi.

Mallya: Mheshimiwa naomba kielelezo namba D1.

Mallya: Soma hapo mwanzoni.

Shahidi: Nilianza harakati za kisiasa na kuwa msaidizi wa Katibu wa CCM.

Mallya: Umemtaja Mrisho Gambo alikuwa chama gani?

Shahidi: CCM.

Mallya: Sabaya alikuwa chama gani?

Shahidi: CCM.

Mallya: Daqaro Mkuu wa Wilaya alikuwa chama gani?

Shahidi: Mkuu wa wilaya hana chama.

Mallya: Unasema Sabaya alikuwa diwani wa chama gani?

Shahidi: CCM.

Mallya: Halafu Magufuli akamteua kuwa mkuu wa wilaya?

Shahidi: Ndiyo.

Mallya: Mwambie Mheshimiwa Jaji Kuwa Mkuu wa Wilaya hana chama ila Magufuli alimteua Sabaya wa CCM.

Shahidi: Ndiyo alimteua akiwa CCM.

Mallya: Hapa karibu umesikia kabla ya Sabaya kufunguwa miaka 30 aliomba Mahakama impunguzie adhabu sababu ana mchumba. Wewe umesema Sabaya alikuwa na mke?

Shahidi: Mimi najua Sabaya alikuwa na mke.

Mallya: Kwa hiyo kule kadanganya Mahakama?

Shahidi: Sijui yeye sasa.

Mallya: Nimesikia ulimtajia Mheshimiwa Freeman Mbowe, Sylvester Nyegu?

Shahidi: Ndiyo.

Mallya: Umesikia kuwa Mahakama imemfunga kwa makosa ya ujambazi Arusha?

Shahidi: Ndiyo. Nimesikia.

Mallya: Soma statement yako hapo mlipokuwa mwishoni mwa mwaka 2017.

(Shahidi anasoma).

Mallya: Kwa hiyo kati ya hapo na hapa ulisema mwisho mwaka 2018 mahakama ichukue lipi?

Shahidi: Aliyeandika atakuwa amekosea.

Mallya: Soma hapo juu.

Shahidi: Mimi nathibitisha kuwa maelezo haya ni sahihi.

Mallya: Sasa wakati gani tujue upo sahihi? Hapo umethibitisha upo sahihi na leo unasema tuchukue ya leo. Kwamba uliacha kazi kwa Sabaya mwaka 2017 na leo unasema aliacha kazi 2018?

Mallya: Hapo chini maelezo uliyosaini yana maana gani?

Shahidi: Yana maana ya uthibitisho.

Mallya: Mkuu wa wilaya analipwa shilingi ngapi?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Sabaya alikuwa anakulipa shilingi ngapi?

Shahidi: 300,000/-.

Mallya: Alikuwa anatoa wapi?

Shahidi: Sifahamu.

Mallya: Umesema Sabaya alikuwa anaongozana na watu saba au wanane. Je, walikuwa wanalipwa na nani?

Shahidi: Sifahamu. Walikuwa ni marafiki zake.

Mallya: Wakati unatoa majina mwaka 2017 na ukaja kuyatoa tena mwaka 2018 kwanini ulikuwa nayo?

Shahidi: Walikuwa marafiki zangu.

Mallya: Ulipokamatwa Arusha alikuhoji Afande Mahita?

Shahidi: Ndiyo.

Mallya: Hayo aliyokuhoji umeyatoa hapa Mahakamani?

Shahidi: Ndiyo.

Mallya: Je, umeshawahi kuyatoa hayo maelezo kwa maana karatasi kwa Mheshimiwa Jaji?

Shahidi: Siyo kazi yangu.

Mallya: Mheshimiwa Jaji naomba ajibu swali langu.

Jaji: Je, aliyatoa lakini?

Mallya: Nataka iingie kwenye rekodi za Mahakama.

Mallya: Ulipokutana na Mbowe gerezani alikuambia nimekuja kuwatoa na kesho yake ukatoka kweli?

Shahidi: Ni sahihi. Nilitoka.

Mallya: Baada ya Kututiwa kesi ulienda Central kufuata vitu vyako?

Shahidi: Ni sahihi. Nilienda Central kwa Inspector Swila nikatoa maelezo ndiyo nikapewa vitu vyangu.

Mallya: Kwa hiyo Mahakama irekodi kuwa ulipewa vitu vyako baada ya kuandika maelezo?

Shahidi: Ndiyo.

Mallya: Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.

Jaji: Hujamuuliza kama alipotoka gerezani alienda kwa mchumba wake

Mahakama inaangua kicheko.

Jaji: Kesho si unaweza kumaliza mapema? Je, tunaweza kupata shahidi mwingine?

Wakili wa Serikali: Bado hatuna uhakika. Tulikuwa tunahangaika kumpata.

Jaji: Basi jitahidi msijiandae kumkosa.

Jaji: basi naahirisha mpaka kesho saa 3 asubuli ambapo upande wa utetezi watamalizia kuuliza maswali ya dodoso.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!