Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Makonda ametonesha vidonda
Makala & UchambuziTangulizi

Makonda ametonesha vidonda

Spread the love

JE  wajuwa? Paul Makonda amerejea kwenye ulingo wa siasa. Huyo ndiye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Hamashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na tayari ameliamsha dude.

Makonda kapiga ‘bigula’ wanasiasa wote waamke wakimbie mchakamchaka wa kisiasa maana wasipofanya hivyo watakiona cha moto.

Kwanza amewafurahisha CCM. Mawaziri goigoi, wasiowajibika, wasiowasikiliza wananchi na kutatua shida zao wajiandae kuzolewa.

Pili amewaudhi wapinzani; amesema kuanzia sasa hakuna upinzani. Amesema wazi kwamba waliopo ni watoa taarifa, tena wakati mwingine wanatoa taarifa nusunusu. Dawa yake amesema atashuhughulika na wanaovujisha taarifa.

Kuhusu Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, amesema akiruka angani kwa chopa tena  kwa mafuta waliyomchangia watafuata huko huko, akitembea kwa miguu wanaye. Akitumia shangingi na wao wamo iwe bara iwe visiwani. Kwa nini hakuwataja ACT-Wazalendo, NCCR Mageuzi au CUF?

Makonda anajua mchakamchaka wa Mbowe si wa kitoto; unahitaji gwaride la nguvu kumkabili. Ndiyo maana ili aweze kufanikiwa kumdhibiti, amewasilisha ombi hatari na lisilokubalika kwamba polisi wakae kando wakati wa mchakamchaka wa kukabili upinzani.

Katika hili Makonda anaturudisha nyuma. Machi 2017 alipokuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, aliwahi kuvamia kituo cha Clouds Media, na kufanya vurugu akiwa na mabaunsa wake. Polisi walikaa kando, hadi sasa hawataki kumfikisha kortini.

Makonda huyu ndiye alifanya sherehe na polisi akiwapongeza kwa kufanikisha uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Ukonga mwaka 2018 uliompa ushindi Mwita Waitara aliyehamia CCM baada ya kuondoka Chadema. Kitendo hicho kiliwakasirisha wengi akiwemo aliyekuwa mwenezi wakati huo Humphrey Polepole.

Halafu katika kipindi hicho akiwa mkuu wa mkoa, ofisa mmoja asiyejulikana, alimnyoshea bastola Nape Nnauye wakati anashuka kwenye gari ili azungumze na wanahabari kule Court Yard. Aliokolewa na waandishi. Polisi waliokuwepo walikaa kando. Hadi leo wamekaa kando.

Polisi walikaa kando kuhusu kupotea kwa Ben Saanane aliyekuwa msaidizi wa Mbowe. Bado wamekaa kando.


Mpaka leo hakuna maelezo ya kina “jinni” gani lilimchukua Leopold Lwajabe, Mkurugenzi wa miradi ya Umoja wa Ulaya nchini (EU) katika Wizara ya Fedha na Mipango kutoka Dar es Salaam na kumpeleka Mukuranga ambako alikutwa kafa.

Kwa hiyo Makonda anapoomba polisi wakae kando anatonesha vidonda wakati hatuoni msaada wa polisi kuwasaka waliomteka Azory Gwanda, mwandishi wa Mwananchi mkoani Lindi na  wasiojulikana waliommiminia risasi Tundu Lissu alipokuwa bungeni Dodoma.

Wakati Rais Samia Suluhu Hassan anafanya mikakati ya kuhakikisha jeshi la polisi linatimiza wajibu wake kwa weledi kulinda amani na kutenda haki, Makonda anataka jeshi la polisi likae kando.

Makonda asiwafikishe watu wakasema “liwalo na liwe”. Endapo hajui basi kinachotokea Israel ni matokeo ya Wapalestina chini ya vyama vyao vya Hamas (kinachotawala Gaza) na Fatah (Ukingo wa Magharibi) kusema liwalo na liwe. Wanajua nguvu ya Israel na misaada mikubwa kutoka Marekani lakini wamesema liwalo na liwe. Tusiende huko!

Mwandishi wa Makala haya ni Joster Mwangulumbi anapatikana kwa simu namba 0753626751

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

Habari za SiasaTangulizi

Gesi asilia, petroli kodi juu

Spread the loveWaziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amependekeza kufanya marekebisho kwenye...

error: Content is protected !!