Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Habari Majaliwa aelezea sekta ya madini inavyoimarika
Habari

Majaliwa aelezea sekta ya madini inavyoimarika

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi na kuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa ambapo hadi sasa imechangia asilimia 7.9 ya pato la taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumatano, tarehe 23 Februari 2022, wakati akifunga Mkutano wa Kimataifa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2022, uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Amesema mchango huo umetokana na jitihada zilizofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa madini, ushirikiano baina ya wadau pamoja na sera nzuri na mazingira rafiki yaliyowekwa na Serikali kwa wawekezaji.

“Kuimarika kwa utendaji pamoja na mambo mengine kumekuwa ni chachu ya mafanikio hata sasa sote tumeshuhudia kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 7.9,” alisema Majaliwa

“Nitoe wito kwa watendaji wote wa sekta ya madini kuongeza juhudi katika utendaji wenu ili sekta hii iweze kuimarika zaidi na hatimaye iweze kuvuka lengo la asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo 2025 kama ilivyobainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa.”

Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kutumia rasilimali ya madini kwa manufaa ya nchi na kuboresha uendeshaji wa shughuli za madini hapa nchini. “Ili kufikia lengo hilo, ni dhahiri kuwa ipo haja kubwa ya kujenga mazingira wezeshi ili sekta hii iweze kuimarika zaidi kwa manufaa ya nchi yetu.”

Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anapenda kuona sekta ya madini inakuwa nguzo muhimu ya uchumi wa nchi na ndio maana ameendelea kuipa umuhimu wa kipekee sekta hiyo kwa kutoa miongozo ambayo imeendelea kuiboresha sekta hiyo ya madini.

“Kipekee nimpongeze sana Rais kwa kuendelea kuhakikisha kuwa wadau wa sekta ya madini, wawekezaji na wachimbaji wadogo wanapata huduma kupitia maelekezo yake. Hii ni dhamira ya dhati ya Serikali yake ya awamu ya sita katika kukwamua na kuendeleza sekta hii.”

Waziri Mkuu ameipongeza wizara ya madini, kwa kuendelea kuandaa makongamano yanayowakutanisha wadau wa uchimbaji wa madini na Serikali, jambo ambalo limechangia kukua kwa sekta hiyo na kutoa wito kwa Wizara kuhakikisha, inaongeza jitihada na kupanua wigo wa ushirikiano baina ya wadau na Serikali.

Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya madini iendelee kuimarisha mifumo ya mawasiliano na wadau wa madini ili iweze kushughulikia kero zinazojitokeza na kuzitatua kwa wakati.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuboresha taasisi zilizo chini yake ili ziweze kutoa huduma nzuri zaidi kwa wachimbaji ikiwa ni pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuendelea kuongeza mitambo ya kuchorongea miamba ambayo itatoa huduma za uchorongaji miamba kwa wachimbaji wadogo kwa bei nafuu pamoja na kuimarisha masoko ya madini nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko amesema wizara hiyo itaendelea na usimamizi na uratibu wa shughuli zote za uchimbaji wa madini pamoja na kushirikiana na wadau ili kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha Watanzania.

Awali, akitoa salamu kwa uwakilishi wa mawaziri waalikwa kutoka Nje ya Nchi, Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi, Ibrahimu Uwizeye, amesema Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika sekta ya madini na Tanzania imekuwa darasa kubwa kwa nchi jirani kutokana na mafanikio makubwa yaliyotokana na uchimbaji wa sekta ya madini.

1 Comment

 • Masoko ya madini yadhibitiwe hasa kwa kutokuweka bei kwenye Vito na Madini….hii ni tabia mbaya..
  Muuzaji anakwmbia ukinuua kwa bei hii ni pamoja na kodi na rising.
  Ukinunua kwa bei nyingine, ni pungufu na bila kodi.
  TAKUKURU waingie kwenye maduka hayo na kujifanya waunuzi. Wasipoona bei kwenye madini, mikufu, Pete, wawapige faini. …
  Wahudhurie darasa la “price display mandatory”
  Mama kaza kama isilegee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

HabariHabari Mchanganyiko

CRB yashtukia makandarasi wanaofanya ubia wa ujanja ujanja, yasema watakaobainika kuchukuliwa hatua kali

Spread the love  BODI ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imeonya makandarasi wanaofanya...

HabariKimataifa

Aliyesomeshwa na mchumba aamuriwa kurudisha Sh 9.4 Mil. baada ya kukataa kuolewa

Spread the love  MWANAMKE mmoja nchini Uganda ambaye aliuumiza moyo wa mchumba...

Habari

Mnyika aacha ujumbe msibani kwa kada wa Chadema aliyefia vitani Ukraine

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema Taifa, John...

HabariHabari Mchanganyiko

Mwili wa kada wa Chadema aliyefia vitani Ukraine wawasili, kuzikwa Mbeya

Spread the loveMWILI wa Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema, aliyefia...

error: Content is protected !!