Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari Kigogo Chadema aliyefutiwa kesi atakiwa kuripoti Polisi Machi 9
Habari

Kigogo Chadema aliyefutiwa kesi atakiwa kuripoti Polisi Machi 9

Spread the love

 

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limemuachia kwa dhamana Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema, Hashim Issa Juma, aliyekamatwa kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi mtandaoni na kumtaka aripoti kituoni hapo tarehe 9 Machi 2022. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 23 Februari 2022 na Wakili wa Juma, Hekima Mwasipu, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.

Juma alikamatwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, kumuondolea mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yanamkabili.

Wakili Mwasipu amedai kuwa, Juma alikamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma zilezile alizokuwa nazo mahakamani hapo.

“Ameachiwa kwa dhamana, ameambiwa aripoti tarehe 9 Machi 2022, wiki mbili kuanzia leo. Kosa ni lile lile alilotenda la kutamka maneno ya uchochezi kwenye mtandao,” amedai Wakili Mwasipu.

Wakili Mwasipu amedai kuwa, DPP aliamua kuiondoa kesi iliyokuwa inamkabili Juma mahakamani hapo, baada ya upelelezi wake kutokukamilika.

Amedai, tarehe 24 Novemba 2021 wakati kesi hiyo inaahirishwa kutokana na upelelezi kutokukamilika, aliiomba mahakama iuamrishe upande wa mashtaka kuja na hati kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), ikiomba ongezeko la muda wa upelelezi.

“Nilivyoenda mahakamani niliwaambia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, inasema ndani ya siku 60 upelelezi wa kesi uwe umekamilika na kesi imesikilizwa, lakini hawakufanya hivyo. Siku zimefika upelelezi haujakamilika, nikasema waje na hati ya kuthibitisha kutoka kwa RCO,” amedai Wakili Mwasipu na kuongeza:

“Kwa uzoefu wangu mimi kesi imeshaisha, kesi za kisiasia zinaishia Polisi.”

Mapema leo, mbele ya Hakimu mMkazi, Mbuya, Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakonho, aliieleza mahakama hiyo kuwa, DPP kwa kutumia mamlaka aliyopewa na kifungu cha 90 (1), cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, amemuondolea Juma mashtaka hayo.

Katika kesi hiyo, Juma alikuwa anakabiiwa na mashtaka mawili ya uchochezi, ambayo ni kuchapisha taarifa ya uongo kwa njia ya kompyuta na kusambaza katika mtandao wa YouTube, kwa lengo la kumchafua na kumdhalilisha Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Simon Sirro.

Alikuwa anadaiwa kumtuhumu IGP Sirro kuwa ni gaidi namba moja, nchini Tanzania na fisadi, wakati si kweli.

Shtaka la mwisho lililokuwa linamkabili ni uchochezi kinyume na kifungu cha 52 (1) na 53 (1), cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, kufuatia kumuita IGP Sirro ni gaidi namba moja na fisadi, mitandaoni.

Alikuwa anadaiwa kutenda makosa hayo tarehe 1 Oktoba 2021, katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza tarehe 7 Oktoba mwaka jana.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

HabariSiasa

Dk. Rose Rwakatare atoa kadi 500 kila Wilaya Morogoro

Spread the loveMWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk...

ElimuHabari

CBE, WMA wasaini makubaliano wanafunzi kusoma wakifanyakazi

Spread the loveNAIBU Spika Musa Azzan Zungu amekipongeza Chuo cha Elimu ya...

HabariTangulizi

Dk. Slaa, Mwabukusi kuhojiwa na jeshi la Polisi Mbeya

Spread the loveJESHI la Polisi jijini Mbeya, linawashikilia kwa mahojiano Dk. Wilbroad...

HabariHabari Mchanganyiko

Kairuki Hospital Green IVF  yawanoa madaktari kuhusu upandikizaji mimba

Spread the love KITUO cha Upandikizaji Mimba cha Kairuki Hospital Green IVF...

error: Content is protected !!