December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Wakili wa Jamhuri ahoji maumivu aliyopata mshtakiwa

Spread the love

 

WAKILI wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, amemhoji shahidi katika kesi ndogo inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, Adam Kasekwa, kama aliweza kuvumilia majeraha aliyopata baada ya kuteswa akiwa mahabusu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wakili Chavula alihoji swali hilo jana Ijumaa, tarehe 25 Septemba 2021, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, mkoani Dar es Salaam, mbele ya Jaji Mustapha Siyani, wakati kesi hiyo ndogo inasikilizwa.

Baada ya Kasekwa ambaye pia ni mshtakiwa wa pili, katika kesi ya msingi ya uhujumu uchumi, akiongozwa na wakili wake, John Mallya kutoa ushahidi, alidai aliteswa alipokuwa mahabusu, ikiwemo kwa kuchomwa na bisibisi maeneo ya makalioni.

Pia, Kasekwa alidai mateso hayo yalimsababishia majeraha madogo maeneo ya makalioni.

Kasekwa aliyekamatwa na mshtakiwa wenzake, Mohammed Abdillah Ling’wenya, tarehe 5 Agosti 2020, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro, aliwahi kuwa komandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kufuatia madai hayo ya kuteswa, Wakili Chavula alimhoji Kasekwa, kwa kuwa yeye ni komandoo aliyefuzu na kwamba miongoni mwa mafunzo aliyofuzu ni kuvumilia hali ya mateso, ambaye alijibu akidai ndiyo.

Wakili Chavula alimhoji Kasekwa, akidai majeraha hayo yalikuwa madogo ndiyo maana aliyavumilia.

Lakini shahidi huyo alijibu akidai, yalikuwa kitu kikubwa ndiyo maana akaieleza mahakama.

Baada ya mahojiano hayo, Jaji Siyani aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, tarehe 27 Septemba 2021.

Kesi hiyo ndogo ilitokana na mapinganizi ya Mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, wakipinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi ya msingi, Adam Kasekwa, yasitumike mahakamani hapo kama kielelezo cha upande wa mashtaka, katika kesi ya msingi, wakidai yalichukuliwa nje ya muda kisheria.

error: Content is protected !!