October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwandishi wa habari mbaroni kwa tuhuma za ugaidi

Spread the love

 

MWANDISHI wa habari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sosthène Kambidi amekamatwa na maofisa wa Jeshi la nchi hiyo na kuhojiwa kwa tuhuma za kushiriki mauaji yaliyofanyika mwaka 2017 kwa wataalam wawili wa Umoja wa Mataifa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mwandishi huyo anayeripoti katika Mashirika la Habari la Ufaransa (AFP, RFI), Reuters na mengine ndani ya nchi hiyo, amekatwa mapema wiki hii akiwa hotelini kutokana na mauaji hayo ya Michael Sharp raia wa Marekani na Zaida Catalan aliyekuwa raia wa Sweden.

Sharp na Catalan walikuwa wakifanya uchunguzi kuhusu makaburi ya halaiki pia walikuwa wakichunguza uhalifu na uasi uliokuwa umeghubika jimbo la Kasai nchini DRC lakini wawili hao walitekwa pamoja na raia wa Congo kisha kuuawa.

Miili ya Sharp aliyekuwa mratibu wa kundi hilo na mtaalamu wa silaha na Catalan ambaye alikuwa mtaalamu wa masuala ya haki za binadamuu, iligunduliwa katika kaburi na wanajeshi wa kulinda amani wiki kadhaa baada ya kutoweka.

Aidha, Wakili wa Mwandishi huyo wa habari, Gode Kabongo ameueleza mtandao wa Aljazeera kuwa Kambidi alikamatwa Jumatatu kisha akaanza kuhojiwa Jumatano wiki hii.

Sosthene Kambidi

“Anashtakiwa kwa makosa kadhaa, ikiwa ni pamoja na kujiunga na kundi la wahalifu, ugaidi na uasi. Nilimwona na kuhudhuria mahojiano yake kwa zaidi ya saa sita. Ninaweza kusema kuwa yuko sawa, ingawa katika jela mtu anaishi katika mazingira magumu,” amesema wakili huyo.

Amesema katika mahojiano hayo, wanajeshi hao wanamshuku kwa kuwa alikuwa akiripoti kuhusu mauaji ya raia katika majimbo ya Kasai na alishiriki katika uchunguzi wa mauaji ya wataalam wawili wa Umoja wa Mataifa, Michael Sharp na Zaida Catalan.

Aidha, Wakili Kabongo ameongeza wanajeshi hao wamemlazimisha aeleze chanzo cha kupata video ya mauaji ya watalaam hao.

Amesema kesi yake inatarajia kuanza ndani ya siku mbili au tatu zijazo katika mahakama ya kijeshi nchini humo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo, ikiwamo Amnesty Internation yamepinga kukamatwa kwake.

Mwandishi huyo ni mwandishi wa pili kutuhumiwa kushiriki mauaji hayo kwani mwandishi mwingine wa habari alikamatwa Julai mwaka huu kwa kuvujisha video ya mauaji ya wataalam hao wawili wa Umoja wa Mataifa.

error: Content is protected !!