October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Butiku atema cheche, akemea ubaguzi wa vyama vya siasa

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku

Spread the love

 

MKURUGENZI Mtendaji na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye mfumo wa vyama vingi vya siasa, ni lazima kuwe na demokrasia sawa kwa maana ya kuwa na uhuru wa kujieleza na kueneza sera za vyama hivyo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Pia amesema ili kuwa na nchi imara ni lazima kusimamia misingi ya katiba na sheria za nchi bila kuendekeza ubaguzi kwa chama kingine au kuwabeza wale ambao hawajashika dola.

Butiku ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Septemba 2021 katika ufunguzi wa mdahalo wa kitaifa wenye kauli mbiu ya “Tushiriki pamoja kudumisha udugu, uzalendo, uwajibikaji, amani, maridhiano na maendeleo yetu,” katika ukumbi wa mikutano wa Morena Jijini Dodoma.

Amesema pamoja na kuwepo kwa demokrasia ni wajibu wa kila mmoja kuwa mzalendo wa kweli katika kuifia nchi yake kwa misingi ya kuhakikisha inakuwa salama.

Aidha, amesema kuwa haina maana ya kuwa na vyama vingi vya siasa ambavyo havijiendeshi kwa kuzingatia mfumo wa kidemokrasia.

“Ili kuwa na nchi yenye afya ni lazima kuzingatia umuhimu wa kuwa na demokrasia ya kweli ambayo inalenga kuwasikiliza watu wote bila kuwa na ubaguzi.

“Mwalimu Nyerere alitufundisha mambo matatu ambayo ni amani, umoja na maendeleo ya watu wote yanayotokana kazi zao pamoja faida kwa taifa kwa ujumla wake” amesema Butiku.

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema nchi ikiendeshwa kwa mfumo sahihi ni wazi kuwa mfumo huo utatambua haki na utu wa mtu jambo ambalo litafanya mtu atambue umuhimu na haki zake.

error: Content is protected !!