October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mgombea Udiwani ACT-Wazalendo agonga mwamba NEC

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera

Spread the love

 

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetupilia mbali rufaa Mgombea Udiwani wa Kata ya Ndembezi, mkoani Shinyanga, kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Mvano Abdul Iddy, aliyepinga kuenguliwa na Msimamizi wa Jimbo la Shinyanga Mjini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, tarehe 25 Septemba 2021 na Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk. Wilson Mahera, akitoa uamuzi wa rufaa ya mgombea huyo wa ACT-Wazalendo, iliyowasilishwa katika tume hiyo.

“NEC katika kikao chake cha tarehe 24 Septemba 2021, ilijadili na kutoa uamuzi kuhusu rufaa iliyowasilishwa na Iddy, dhidi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini.

“Katika rufaa hiyo mrufani alikuwa akipinga uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi kutengua uteuzi wake kutokana na pingamizi lililowekwa na Mgombea wa CCM, Victor Thobias Mmanywa,” imesema taarifa ya Dk. Mahera.

Taarifa ya Dk. Mahera imesema, uamuzi huo umechukuliwa baada ya NEC kujiridhisha kwamba nyaraka zilizowasilishwa na mrufani hazikuwa na uthibitisho wa kuonesha kuwa alitoa tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi, mbele ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi.

“Kanuni zinazotakiwa kuzingatiwa ni kanuni ya 24 (6) ya Kanuni za Uchaguzi wa Madiwani za 2020, ikisomwa pamoja na kipengele cha 14 cha Maadili ya Uchaguzi ya Rais, Wabunge na Madiwani ya 2020,” imesema taarifa ya Dk. Mahera na kuomgeza:

“NEC kwa mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, kikisomwa pamoja na kanuni ya 30 (3) ya Kanuni za Uchaguzi wa Madiwani za 2020, imekataa rufaa hiyo na imekubaliana na uamuzi wa msimamizi wa Uchaguzi katika Kata ya Ndembezi wa kutengua uteuzi wake.”

Uchaguzi mdogo wa Kata ya Ndembezi unatarajiwa kufanyika tarehe 9 Oktoba 2021, pamoja na chaguzi zingine ndogo katika kata tisa na majimbo mawili.

error: Content is protected !!