Sunday , 5 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe: Kilichowakimbiza Lissu, Lema Tanzania chatajwa
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe: Kilichowakimbiza Lissu, Lema Tanzania chatajwa

Spread the love

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chadema-Bara nchini Tanzania, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Goodbless Lema, wanadaiwa kwenda kuishi uhamishoni kwa sababu ya kukosa ulinzi baada ya walinzi wao kuwa mahabusu wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Madai hayo yametolewa leo Jumanne, tarehe 1 Februari 2022, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam mbele ya Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo.

Ni wakati Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Utetezi, Peter Kibatala katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake anamuuliza maswali ya dodoso shahidi wa Jamhuri, Luteni wa JWTZ, Denis Urio.

Mbali na Mbowe washtakiwa wengine katika kesi hiyo yenye mashtaka sita ya ugaidi ni waliokuwa makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Makomando hao wanaodaiwa kufukuzwa kazi JWTZ kwa sababu za utovu wa nidhamu, walikamatwa katika nyakati tofauti Agosti 2020, Kilimanjaro na Dar es Salaam, kwa tuhuma za ugaidi, ikiwemo kukutwa na silaha, vifaa na sare za JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kinyume cha sheria.

Na nyingine ni kupanga njama za kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, kuchoma vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu.

Kwa sasa Sabaya ni mfungwa katika Gereza la Kisongo mkoani Arusha, akitumikia miaka 30 pamoja na wenzake.

Wakili Kibatala alimuuliza Luteni Urio, kama anafahamu wenzake Mbowe ni miongoni mwa makomando walipangwa kwenda kumlinda Lissu na Lema baada ya kupata tishio la kiusalama, ambapo alijibu akidai hafahamu.

Mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo;

Kibatala: Unamfahamu Goodbless Lema?

Shahidi: Namsikia.

Kibatala: Unafahamu amehama nchini baada ya kupata matishio ya kiusalama?

Shahidi: Sina uhakika, sifahamu.

Kibatala: Unafahamu Lissu aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema mpaka leo anaishi uhamisho kwa sababu ya kuhofia usalama wake?

Shahidi: Sina uhakika kama anaishi nje kwa sababu ya usalama wake.

Kibatala: Unafahamu anaishi uhamishoni?

Shahidi: Kama ameenda kutembea? Sabaabu si alirudi katika uchaguzi.

Kibatala: Unafahamu kama anishi uhamishoni hufahamu?

Shahidi: Sina uhakika.

Kibatala: Unafahamu kama hawa vijana watatu wasingekamatwa Lissu asingeondoka, sababu hawa na wengine wangekuwa wanatoa ulinzi kwake?

Shahidi: Kwani walikamatwa kwa kuonewa? Mi najua walikamatwa kwa kufanya uhalifu, umefanya uhalifu utakamatwa.

Kibatala: Unafahamu kwamba moja wapo ya sababu za kiusalama zilizopelekea Lissu kuondoka, pamoja na matishio mengine ya kiusalama amenyang’anywa walinzi wake wako mahakamani wanshtakiwa, unafahamu hufahamu?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unafahamu pia kwamba, hata Lema naye ameondoka kwa sababu hizo?

Sababu moja wapo ya vijana hawa ilikuwa apelekwe kwa Lema na saa hana ulinzi ikabidi akimbie kule sababu ya matishio ya usalama kwake?

Shahidi: Sifahamu.

Lissu yuko uhamishoni nchini Ubelgiji, tangu 2017 alikokwenda kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba mwaka huo, jijini Dodoma.

Lakini Julai 2020 alirudi kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, ambapo alipitishwa na Chadema kugombea urais wa Tanzania. Baada ya kushundwa katika uchaguzi huo, Novemba 2020 alirejea nchini humo akidai amepata tishio la kiusalama.

Naye Lema alienda kuishi uhamishoni nchini Canada, baada ya uchaguzi huo kumalizika akidai alipata tishio la kiusalama.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Tanzania lilikanusha madai yao na kuwataka wanasiasa hao warejee nchini likiwaahidi kuwapatia ulinzi.

Luteni Urio amemaliza kutoa ushahidi wake aliouanza Jumatano iliyopita.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Ijumaa, tarehe 4 Februari 2022.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga Hidaya chatikisa Mafia

Spread the loveWAKATI hali ya upepo mkali ikiendelea kushuhudiwa katika baadhi ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mbatia ambwaga Selasini, mahakama yaamuru alipwe fidia

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemuamuru...

Habari za SiasaTangulizi

Mkulo afariki dunia, kuzikwa kesho Kilosa

Spread the loveALIYEKUWA Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kilosa (CCM), Mustafa...

Habari MchanganyikoTangulizi

Usafiri baharini wasitishwa kukwepa athari za kimbunga Hidaya

Spread the loveUSAFIRI wa baharini umesimamishwa kwa muda ili kukwepa athari za...

error: Content is protected !!