Monday , 27 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Kesi ya Lulu yaunguruma, mdogo wa Kanumba atoa ushahidi
Habari MchanganyikoMichezo

Kesi ya Lulu yaunguruma, mdogo wa Kanumba atoa ushahidi

Spread the love

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imeanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya mauaji ya bila kukusudia, inayomkabili msaanii wa filamu nchini, Elizabeth Maichael (Lulu), dhidi ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, anaandika Faki Sosi.

Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Seth Bosco (30) ambaye ni ndugu wa marehemu Kanumba, ameeleza mahakama kuwa Lulu na kaka yake walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Mbele ya Jaji wa Mahakama hiyo, Sam Rumanyika, wakili mkuu wa serikali, Faraja George alimuungoza shahidi huyo na kusema, “upande wa mashitaka umepanga kuleta mahakamani mashahidi watano ili kujenga kesi yake.”

Alisema, miongoni mwa mashahidi wa Jamhuri, ni pamoja na daktari wa Kanumba (Dk. Paplas). Shahidi huyo alitarajiwa kuanza kutoa ushahidi wake leo (Alhamisi), lakini kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kiafya ameshindwa kufanya hivyo.

Mbele ya mahakama, Bosco ambaye alikuwa akiishi nyumba moja na Kanumba Sinza jijini Dar es Salaam alisema, yeye ni ndugu wa marehemu na kwamba alikuwa akiishi nyumbani kwa msanii huyo.

Alisema anamtambua Lulu kama rafiki wa kaka yake na kwamba tarehe 16 Aprili mwaka 2012, tokea asubuhi, alikuwa nyumbani kwa Kanumba. Alisema, alipanga kuondoka saa 10 alasiri, lakini kaka yake akamuomba amsubiri ili waweze kutoka wote saa sita usiku.

Amedai kuwa ulipokaribaribia muda wa waliokubalina kuondoka (saa sita usiku), aliamua kuingia bafuni kwa ajili ya kuoga ili kujiandaa na baada ya kumaliza, naye Kanumba aliingia bafuni.

Alisema, “mimi nilikuwa wa kwanza kumaliza kujiandaa. Baada ya Kanumba kumaliza kuoga, muda mfupi baadaye Lulu alifika nyumbani akiwa na gari ambalo alikuwa akiliendesha yeye mwenywe.”

Bosco alisema, “haraka Kanumba alienda kumfungulia mlango na kuingia naye chumbani kwake, lakini wakati wakiwa kwenye korido walianza kulumbana.”

Anasema, moja ya malumbano yao yalihusu tuhuma kuwa Lulu amepokea simu ya rafiki yake mwingine wa kiume mbele ya Kanumba.

Bosco ameeleza mahakamani kuwa mzozo huo uliendelea mpaka chumbani kwa Kanumba ambako aliendelea kusikia sauti za wawili hao wakigombana.

Ameiambia mahakama kwamba muda mchache baadaye, Lulu alikimbilia chumbani kwake na kumueleza kuwa Kanumba amedondoka bila kufahamu kilichosababisha kuanguka kwake.

Shahidi huyo amedai kuwa alikwenda chumbani kwa Kanumba na kumkuta akiwa kwenye hali mbaya huku ameegemea ukuta.

Ameeleza kuwa kwenye ukuta alipodondoka Kanumba aliiacha alama kwa kuwa alikuwa amepaka Superblock kwenye nywele zake.

Upande utetezi uliowakilishwa na wakili, Peter Kibatala, ambaye alimuuliza shahidi huyo maswali kadhaa kutokana na ushahidi aliyoutoa.

Mahojiano kati ya wakili Kibatala na Bosco yalikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala: Maneno ya kuzozona kati ya marehemu na mshitakiwa ulikuwa unayasikia ukiwa chumbani au kwenye korido.

Shahidi: Nilisikia kuanzia kwenye korido na wakiendelea kwenda chumbani kwake.

Kibatala: Wakati hiyo simu iliyopelekea ugomvi ikiita uliisikia?

Shahidi: Sikuisikia.

Kibatala: Ni kweli kwamba wewe na mshitakiwa mlikuwa mnaishi kama mtu na shemeji yake ambapo mlizoeana na kuishi pamoja kiasi ambacho unaweza kukumbuka mlio wa simu ya shemeji yako?

Shahidi: Sikumbuki.

Kibatala: Ni kweli au siyo kweli kwamba wakati ugomvi ukiendelea ulikuwa kwenye mlango wa Kanumba ukitaka kujua mzozo huo.

Shahidi: Siyo kweli.

Kibatala: Ni kweli au siyo kweli ulimsikia mtuhumiwa akilia wakati mzozo ule ukiendelea huku akitaka kutoka kwenye chumba cha Kanumba?

Shahidi: Siyo kweli.

Kibatala: Ni kweli kwamba ugomvi wa namna hiyo haukuwa wa kwanza kutokea kati ya mtuhumiwa na marehemu.

Shahidi: Siyo kweli.

Kibatala aliiomba mahakama kumkabidhi shahidi maelezo aliyoyatoa polisi na kuiambia ikubali kuyapokea kama kielelezo.

Baada ya shahidi kurejea tena kusoma maelezo yake Kibatala aliendelea.

Naomba umueleze mheshimiwa Jaji kwa mujibu wa maelezo yako uliyoyatoa ulipokuwa ukihojiwa polisi, kuwa zile kelele zilizozua mzozo kati ya Kanumba na mshitakiwa zilikuwa zinatoka chumbani kwa Kanumba na siyo kwenye korido.

Shahidi: Nilizisikia kutoka kwenye chumba cha Kanumba.

Kibatala: Mueleze jaji kuwa ulimsikia mshtakiwa akilia alipokuwa akizozana na Kanumba.

Shahidi: Wakati huo nilisikia sauti za majibizano.

Kibatala: Nilipokuuliza kuwa uliposikia kelele hizo ulijaribu kufungua mlango wa Kanumba ukanijibu siyo kweli mara mbili ukiwa chini ya kiapo, lakini mueleze Jaji kwa mujibu wa maelezo yako uliyoandika siku chache baada ya tukio ulipohojiwa na polisi.

Shahidi: Nilijaribu kufungua mlango.

Baada ya hapo baraza la wazee wa mahakama walipata fursa ya kuuliza maswali kwa shihidi.

Mzee wa baraza Na. 1 aliuliza: wakati mtuhumiwa anashuka kwenye gari ulimuona anashuka na kitu gani ambacho kinaweza kudhuru?

Shahidi: Sijamuona akishuka na kitu chochote.

Mzee wa baraza Na 2 akauliza: wakati mshtakiwa anashuka aliongozana na nani?

Shahidi: Hakuwa ameongozana na mtu yeyote. Alikuwa pekee yake.

Naye mzee wa baraza Na 3 akahoji: Kulikuwa na ugomvi wowote kati ya marehemu na mshtakiwa?

Shahidi: Hapana tulikuwa tunaishi vizuri.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kesho. Mahakama imeamua kesi hii kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo Alhamisi, tarehe 19 Oktoba 2017.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Wazanzibar watarajia makubwa kutoka NMB Pesa Akaunti

Spread the loveWateja wapya wa Benki ya NMB wa Zanzibar wanatarajia neema...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kinana aungana na Tale kugawa mitungi ya gesi 800

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman...

Habari MchanganyikoMichezo

NBC yakabidhi Kombe la Ubingwa wa Vijana (U20) kwa Kagera Sugar FC

Spread the loveMdhamini mkuu wa Ligi ya Vijana chini ya miaka 20...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Madeni ya bilioni 219 yalipwa, wadai wengine waitwa

Spread the loveSERIKALI imesema kuanzia Mei mwaka 2021 hadi sasa imelipa madai...

error: Content is protected !!