Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Katiba ya CCM yarekebishwa, Samia atoa neno
Habari za Siasa

Katiba ya CCM yarekebishwa, Samia atoa neno

Spread the love

 

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamepitisha mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya chama hicho Taifa (NEC), kuhusu marekebisho ya katiba ya 1977, toleo la 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mapendekezo hayo yaliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, yamepitishwa leo Ijumaa, tarehe 1 Aprili 2022, kwenye mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan.

Chongolo amesema mapendekezo hayo yamelenga kufanya marekebisho ya katiba ya CCM, katika sehemu 12, kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa chama hicho.

Akizungumza wakati mapendekezo hayo yanapitishwa na wajumbe, Samia amesema marekebisho hayo yanalenga kuongeza meno uongozi wa CCM ngazi ya kata au wadi , kwenye usimamizi wa miradi ya maendeleo, inayotekelezwa na Serikali kupitia ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Aidha, Samia ambaye ni Rais wa Tanzania, amesema marekebisho ya katiba hiyo ni sehemu ya mchakato wa uchaguzi mkuu wa CCM unaofanyika mwaka huu.

“Bila shaka mtakubaliana na mimi ajenda hizi ni za muhimu sana, sio tu kwa uhai na maendeleo ya chama, bali kwa maendeleo ya Taifa. Mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake, vifungu vinavyofanyiwa marekebisho vinahusika moja kwa moja,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Vifungu vitakavyorekebishwa vitatumika katika kujaza nafasi za wajumbe katika chaguzi mbalimbali za CCM. Kwa mnasaba huo kazi tunazofanya leo ni sehemu ya maandalizi ya chaguzi za chama na jumuiya zake.”

Miongoni mwa marekebisho hayo katika Katiba ya CCM, yamegusa Ibara yake ya 104 (1-11), inayozungumzia kazi za Kamati Kuu ya NEC ya chama hicho, ambapo yameongezwa maneno yanayosomeka “mwenyekiti wa halmashauri ya mji au wilaya”, katika kifungu kidogo cha 7 (h) cha ibara hiyo.

Chongolo amesema madhumuni ya marekebisho hayo ni kuimarisha nguvu ya CCM katika kukabiliana na kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye matumizi ya madaraka.

Mabadiliko hayo pia yamegusa Ibara ya 104 (1-11), inayotoa maelekezo ya kazi za Kamati Kuu ya NEC, kwa kuongeza maneno “makatibu wasaidizi wa idara za makao makuu ya CCM na makatibu wa CCM wilaya” kwenye Ibara ya 104 (6).

Lengo la marekebisho hayo ni kuimarisha udhibiti wa Kamati Kuu ya CCM kwenye usimamizi wa uwajibikaji wa kazi za chama hicho.

Ibara nyingine zilizoguswa na marekebisho hayo, ni ya 102 (1-23), inayozungumzia kazi za NEC, ambapo imeongezwa Ibara mpya ya 102 (12)(k), kwenye Ibara ya 102 (12A-J), inayosema “kuwateua makatibu wa CCM wa mikoa.”

Chongolo amesema lengo ni kulipa nguvu na uhalali wa kikatiba, pendekezo linalohusu makatibu wa CCM wa mikoa kuwa wajumbe wa NEC.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan

Ibara nyingine zilizoguswa na marekebisho hayo ni ya 101 (1)(a) hadi (w), inayohusu wajumbe wa NEC Taifa, kwa kuongeza Ibara mpya ya 101 (1)(x), inayowaongeza makatibu wa CCM wa mikoa.

Nyingine ni, Ibara ya 91 (1-9), inayozungumzia kazi za Kamati ya Siasa ya NEC mkoa, ambapo maelezo ya kifungu chake cha 6(g)yamefutwa na kuandikwa upya yanayosomeka “kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya NEC Taifa, juu ya majina ya wanachama wa CCM watakaogombea nafasi za

Mameya wa Jiji na Manispaa na wenyekiti wa halmashauri za miji na wilaya.”

“Pia kufanya uteuzi wa mwisho kwa wanachama wa CCM watakaogombea nafasi za manaibu meya kwa halmashauri za majiji na manispaa.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!