ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mzee Phillip Mangula, amemtaka mrithi wake, Abdulrahman Kinana, kuwashughulikia WanaCCM wanaokiuka maadili kwa kuanza mapema mikakati ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Mzee Mangula amempa maelekezo hayo Kinana, leo Ijumaa, tarehe 1 Aprili 2022, jijini Dodoma, muda mfupi baada ya Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, kumpitisha kwa asilimia 100 kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara.
“Ile kamati ndogo ya udhibiti nakukabidhi Kinana, utakuwa ndiyo mzee wa mafaili. Kwa nini mzee wa mafaili, hivi sasa tumeanza kuangalia wanaochungulia 2025. Ukiona tu kuna dalili fulani unafungua faili, unaanza kuweka kumbukumbu, huyu kasema hiki,”
“Kila mmoja anayeonekana kukiuka taratibu unamfungulia faili ili kuweka kumbukumbu za kinyume na maadili, hayo nimekukabidhi bila shaka unayafahamu pia.”
Akizungumzia kung’atuka kwake katika wadhifa huo, Mzee Mangula amesema hatua hiyo haimaanishi kwamba atajitenga na shughuli za CCM, kwani ataendelea kutekeleza majukumu yake akiwa mjumbe wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu.
“Lakini kung’atuka kwangu haimaanishi kutoka kwenye shughuli na uongozi wa chama, kwa nini nasema sitoki? Kwasababu kuna Baraza la Ushauri linaloundwa na viongozi wakuu wastaafu na mimi kuanzia sas ani mjumbe,” amesema Mzee Mangula.
Mzee Mangula amesema aliamua kung’atuka nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, kwa kuwa umri wake ulikuwa unafaa kuwa katika baraza hilo la wastaafu.
“Ibara ya 122 inasema kutakuwa na Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu, wajumbe wote watakuwa wazee kuanzia miaka 60 wanaokubali imani, malengo na madhumuni ya CCM, nikija huko nakuja kama mzee wa miaka hiyo, inaanzia 60 niko 80 nastahili kuwa kwenye baraza,” amesema Mzee Mangula.
Leave a comment