Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Hamad Rashid asimulia Nyerere alivyomuonya kulinda Muungano, ataja mambo 3
Habari za Siasa

Hamad Rashid asimulia Nyerere alivyomuonya kulinda Muungano, ataja mambo 3

Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed
Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed amesema miaka michache baada ya kutimuliwa ndani ya CCM na kwenda kumtembelea Mwalimu Julius Nyerere, Baba huyo wa Taifa alimuonya kuangalia uhai wa muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

Hamad Rashid ambaye mwaka 1985 alitimuliwa CCM yeye na viongozi mbalimbali akiwamo Maalim Seif Sharif Hamad, Juma Duni Haji, amesema baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza mwaka 1992, walimpelekea Mwalimu Nyerere, kanuni na Katiba ya CUF – chama ambacho walikiasisi.

Akizungumza leo tarehe 9 Aprili, 2022 katika mdahalo wa kitaifa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Hayati Mwalimu Nyerere, Rashid amesema Mwalimu Nyerere aliwasisitiza kwa kuwataja kwa majina kwamba licha ya kuwa viongozi wa upinzani wasiende kuuvunja Muungano.

Rashid amesema enzi za uongozi wa Baba wa Taifa alikuwa na utashi si wa muungano tu wa Tanzania bali pia kuona Afrika inakuwa nchi moja.

“Lakini Mwalimu aliona ni rahisi kuwe na ushirikiano wa kikanda kwanza. Kitu kikubwa ilikuwa utashi, alihangaikia Shirikisho la Afrika Mashariki ikashindika ndio ikaja Tanganyika na Zanzibar,” amesema.

Amesema kati ya mwaka 1921 – 1963 Zanzibar ilikuwa na vyama zaidi ya 13, vingi vikiwa vya kikabila, kijinsia.

“Kulikuwa na vyama vinaitwa Ndizi, Mgomba, Africa Association, Shiraz Party, mpaka mwaka 1961 tukaja na vyama vikubwa ASP, ZNP baadaye Umma Party, ZPPP, ndivyo viliingia uchaguzi hadi ikaona hamna haki ndipo mapinduzi yakatokea mwaka 1964,” amesema na kuongeza;

“Jambo moja ambalo tunajifunza kwa Mwalimu ni namna alikuwa anatafuta fursa kwamba ni vipi tunaweza kuungana kama Afrika, Kanda au kama nchi.”

Rashid amesema lingine la kujifunza kutoka kwa Mwalimu ni uvumilivu wake.

“Zanzibar baada ya mapinduzi Mzee Karume alisema hakuna uchaguzi Zanzibar mpaka labda baada ya miaka 60. Wakati huo unaendesha uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Zanzibar ukiacha uchaguzi wa Rais hakuna uchaguzi mwingine,” amesema.

Amesema mpaka mwaka 1972 Mzee Abeid Amani Karume alipofariki Mzee Abood Jumbe alipochukua madaraka akaanza utaratibu kuona namna gani Wazanzibar wanaweza kuingia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa idadi kubwa kidogo.

“Baraza la Mapinduzi likaweka utaratibu wa kuchagua wabunge kwenye wilaya wakapatikana wabunge 10 na hatimaye Bunge lenyewe baadaye likaweka utaratibu wa kuchagua kwenye mikoa na mimi nikapata bahati mwaka 1977 kuchaguliwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano kutoka Mkoa wa Kusini Pemba.

“Huu ni uvumilivu mkubwa sana, kwamba huku ni uchaguzi wa watu lakini upande wa pili kuna uchaguzi wa kitaasisi na wewe unazungumzia demokrasia,” amesema.

Amesema jambo la tatu la kujifunza kutoka kwa Mwalimu Nyerere ni kwamba hakuwa mchoyo ndio maana hata baada ya Muunga wa Tanganyika na Zanzibar, Mzee Karume ndiye alimwambia kuwa awe Rais.

Pia wakati akihangaika kuunganisha shirikisho la Afrika Mashariki alikubali kuuachia urais kama wangefanikiwa.

Rashid amesema kuna wakati alimuuliza Mwalimu Nyerere kwanini anaing’ang’ania Zanzibar, akamjibu kuwa Tanzania kuba makabila zaidi ya 120, Zanzibar yapo makabila mengi vilevile, lakini wote tunahitajiana kwani kila upande ukienda kwingine unakuwa na sauti moja.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!