MBUNGE wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani, ameihoji Serikali ya Tanzania, kwa nini wanafunzi wameendelea kuchangishwa michango wakati “inasema elimu ya Shule ya msingi na sekondari ni bure? Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Aida, amehoji hilo, leo Jumatatu, tarehe 7 Juni 2021, bungeni jijini Dodoma, wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
“Je, kwa nini Wazazi wanachangishwa michango ya kuchangia elimu wakati Serikali inasema elimu ya Shule ya Msingi na Sekondari ni bure,” amehoji Aida
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Tamisemi, David Silinde amesema, Serikali kupitia Waraka wa Elimu Namba 5 wa mwaka 2015 iliamua kutoa Elimumsingi bila malipo kuanzia Elimu ya awali hadi Kidato cha Nne.
“Uamuzi huo ulijielekeza katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ambayo ina lengo la kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wenye rika la Elimumsingi wanapata Elimu bila kikwazo chochote ikiwemo Ada au michango,” amesema
Silinde amesema, Serikali ilitoa Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa Elimumsingi Bila Malipo.
“Waraka huu unafafanua maana ya Elimumsingi na kuainisha majukumu ya kila kundi linalohusika katika utoaji wa Elimumsingi bila malipo na kuweka utaratibu wa utekelezaji wake,” amesema
Silinde amesema, majukumu ya jamii na wananchi kuhusu michango yamebainishwa kwenye Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016.
Amesema, Waraka unaeleza kuwa Kamati za Shule au Bodi za Shule zitashirikisha jamii katika maazimio na maamuzi ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na maendeleo ya shule hususan uchangiaji wa hiari na kuwasilisha maamuzi hayo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili kupata kibali.
“Hivyo, uchangiaji katika elimu unaoruhusiwa ni wa hiari na hauhusishi wanafunzi kuzuiwa kuhudhuria masomo,” amesema
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema, kuna michango ya hiari ambayo kupitia kamati za shule, wazazi wana ridhia na kuchangia.
Swali kama hilo la Aida, si la kwanza kuulizwa bungeni, limekuwa likiulizwa mara kwa mara hasa michango inayochangishwa wakati elimu ni bure.
Leave a comment