Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CUF, ACT-Wazalendo hapatoshi, Bwege acharuka
Habari za SiasaTangulizi

CUF, ACT-Wazalendo hapatoshi, Bwege acharuka

Bwege
Spread the love

MGOGORO wa kugombania mali za chama kati ya Chama Cha Wananchi (CUF) na ACT-Wazalendo, umeibuka upya baada ya kusababisha vurugu kati ya wafuasi wa vyama hivyo wilayani Kilwa Kivinje, Mkoa wa Pwani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Vurugu hizo ziliibuka leo tarehe 18 Januari 2024, baada ya baadhi ya wafuasi wa CUF kudaiwa kuvamia eneo la ACT-Wazalendo katika Kiwanja cha Utete A namba 18, Kijiji cha Magengeni, kuzuia ujenzi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Inadaiwa kuwa, kufuatia vurugu hizo, Kiongozi wa Kitengo cha Itifaki CUF Kilwa, Juma Ngondae anashikiliwa na Jeshi la Polisi, huku viongozi wengine 11 wa chama hicho walifungiwa ndani na wafuasi wa ACT-Wazalendo kwa saa kadhaa, kisha kufunguliwa na polisi.

Mgogoro wa kugombea mali kati ya CUF na ACT-Wazalendo, uliibuka 2017 baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Hayati Maalum Seif Sharif Hamad pamoja na wafuasi wake kutimkia ACT-Wazalendo.

Kuibuka kwa taarifa za vurugu hizo, kumekuja baada ya Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, kudai Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud, ambaye ni kiongozi wa ACT-Wazalendo, anataka kulipora eneo hilo ka kutumia cheo chake.

“Wakati taifa likiendelea kujadili kuhusu maridhiano ya kitaifa na siasa za kistaarabu, ACT-Wazalendo kinaendelea na mipango haramu ya kuvamia na kujaribu kupora kwa mabavu eneo la ofisi ya Wilaya ya CUF Kilwa mkoani Lindi.

“Mpango huo unaofahanika na viongozi wakuu wa ACT-Wazalendo unalenga kutumia Dola Kwa kivuli Cha kofia ya umakamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar ambapo Othman amepanga kuzindua ujenzi wa ofisi ya chama hicho kwenye eneo la ofisi za CUF kesho Ijumaa,” imesema taarifa ya Prof. Lipumba.

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo

Taarifa ya Prof. Lipumba inadai kuwa, kabla ya ACT-Wazalendo kutaka kuchukua eneo hilo walifungua kesi Baraza la Ardhi la Wilaya na mahakama ya mkoa, wakashindwa.

“Kwa kile tunachoweza kutafsiri kwamba ni kutaka kusababisha vurugu na umwagaji damu, Januari 7 walivamua eneo letu wakafyeka na Januari 11 walileta mchanga na mashine za kufyatulia tofali. Tukafikisha taarifa kwa mkuu wa wilaya, Christopher Ngubyagai, ambaye alisema ACT-Wazalendo hawana haki ya kuvamia eneo la CUF,”

“Jana mkuu wa wilaya akatuita ghafla na kutengua maamuzi yake yaliyozingatia sheria na kuagiza ACT-Wazalendo wanaruhusiwa kuendelea kufanya ujenzi kwenye eneo hilo la CUF,” imesema taarifa ya Prof. Lipumba.

Kupitia taarifa hiyo, Prof. Lipumba ameviomba vyombo vya Dola kuzuia jaribio ya eneo linalidaiwa kuwa la CUF kuporwa na ACT Wazalendo.

Kutokana na madai hayo, MwanaHALISI ilimtafuta Msemaji wa CUF, Mhandisi Mohamed Ngulangwa kwa ajili ya kujua umiliki wa eneo hilo, ambaye alisema ni la chama chao na kwamba wana hati.

“Unajua tangu mgogoro huu uanze tumekwua na changamoto ya kuporwa maeneo yetu na Kuna kesi kadhaa ziko mahakamani kuhusu suala hilo. Hilo eneo ni la kwetu na hati ya kiwanja tunayo,” amesema Mhandisi Ngulangwa na kuongeza:

“Eneo hilo ni mali ya chama tangu 2015. Na hata kama kuna mtu alilinua akalikabidhi CUF na akaandika katika hati jina la CUF kisheria maana yake ni mali ya CUF. Pia, wao wanataka kujenga ofisi kinyume cha sheria sababu hairuhisiwi vyama viwili kuwa na ofisi sehemu moja.”

Aidha, MwanaHALISI Online ilimtafuta Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, ili kupata maelezo ya chama hicho juu ya mgogoro huo, ambaye alisema suala hilo linashughulikiwa na chama chake ngazi ya wilaya kwa kuwa ndio wanaojus mmiliki halali wa eneo hilo.

“Ushari wangu kwako, hilo suala la wilayani Kilwa, viongozi wa Kilwa Wanaweza kufafanua zaidi sababu wanajua masuala ya historia yake kutokea CUF,” amesema Ado.

Aidha, Ado aliutaka mtandao huu untafute Selemani Bungara (Bwege), akisema ndio mmiliki halali wa eneo hilo.

Bwege alipotafutwa alidai eneo linalobishaniwa ni mali yake, alilinunua kutoka kwa Salum Mkanjima na kwamba ameamua kuwapa ACT-Wazalendo.

Bwege alidai kuwa, mbali ya eneo hilo, aliwapa CUF nyumba yake iliyoko eneo la Ukote A namba 17, kwa ajili ya kufanya ofisi kwa muda hivyo kwa sasa kesi Iko mahakamani ili chama hicho kimrejeshee.

 

“Hilo eneo ni mali ya ACT-Wazalendo na niliyelitoa ni Mimi. Sijalitoa kwa CUF ndio maana tumeenda kwa mkuu wa wilaya wametoa hati yao na sisi tumetoa ya kwetu ikaonekana ni sahihi.

“Kiwanja ambacho nilijenga nyumba yangu ni Ukote A 17, ambayo niliwapa CUF iwe kama ofisi kwa muda na sio nyumba yao na hati yake ninayo. Kama wana malalamiko waende mahakamani kuweka zuio,” amesema Bwege na kuongeza:

“Waulize wao wako sahihi kuja kufanya vurugu katika eneo ambalo sio lao? Wao wanafanya hivyo ili kumzuia Othman Masoud kesho asiende kuzindua jiwe la ujenzi.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!