May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

COVID-19: Prof. Lipumba ‘watu wana hofu’

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

Spread the love

 

PROFESA Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) amesema, wataalamu na wanasayansi Tanzania wamekuwa na hofu ya kueleza hali halisi kuhusu maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19) nchini. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Buguruni jijini Dar es Salaam, leo tarehe 7 Machi 2021 amesema, serikali itumie wanasayansi kukabili virusi vya corona.

“Hasa kwenye magazeti ya nje, watu wanaomba kutotajwa majina yao kutokana na woga wa kuingia matatani.

“Watu wana hofu, wanamashaka, wanaogopa. Tuiondoe hii hofu. Madaktari na wanasayansi waweze kufanya utafiti bila woga,” amesema.

Prof. Lipumba ameishauri serikali kushirikiana na mataifa mengine duniani ili kupata chanjo hiyo.

“Tunatoa wito kwa serikali kufanya utaratibu kwa kuwatumia wataalamu wa afya kufanyia uchunguzi chanjo za corona, hatimaye majibu ya wataalamu na ndio yaongoze uamuzi juu ya kutumia chanjo hizo.

“Tushirikiane na taasisi za kimataifa, tutumie wataalamu na tuwasikilize,” amesema Prof. Lipumba.

Tayari viongozi mbalimbali wa kiroho wamewataka waumini wao kuchukua tahadhari dhidi ya corona.

Hata hivyo, serikali imesisitiza Watanzania kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na virusi hivyo.

Na kuwa, miongoni mwa hatua muhimu ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka.

error: Content is protected !!