May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Mahindi Kenya Vs Tanzania: Zitto aonesha njia

Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo

Spread the love

 

WAKATI Serikali ya Tanzania ikilalamikia hatua ya Kenya kuzuia mahindi yake kuingia nchini humo, Zitto Kabwe ameshauri diplomasia itumieke. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).

Malalamiko ya Tanzania yametolewa leo Jumapili tarehe 7 Machi 2021, na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alipotembelea wafanyabiashara wa mahindi waliozuiwa kuingiza Kenya kupitia mpaka wa  Namanga mkoani Arusha.

Sakata hilo la mahindi ya kuzuiwa kuingia nchini Kenya, liliibuka tarehe 5 Machi 2021 baada ya Mamlaka ya Kilimo na Chakula nchini humo kupiga marufuku mahindi ya Tanzania na Uganda kwa madai ya kutokidhi viwango vya usalama wa chakula cha binadamu.

Kenya imeeleza, mahindi ya nchi hizo mbili yana viwango vikubwa vya sumu ya Mycotoxic.

Akizungumzia sakata hilo, Bashe amesema Serikali ya Tanzania haijapokea taarifa  rasmi juu ya hatua hiyo.

Mahindi yaliyohifadhiwa kwenye viroba tayari kwa kwenda sokoni

“Kama nchi hatujapokea taarifa rasmi ya kiserikali, tunajua wameleta notice (taarifa) upande wao wa boda Namanga kuzuia magari yetu ya mahindi yasivuke upande wa pili.

“Natarajia serikali ya Kenya iwasiliane  na serikali ya Tanzania rasmi,” amesema Bashe.

Zitto ambaye ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo,  ameishauri Serikali ya Tanzania kuzungumza na Serikali ya Kenya ili kumaliza suala hilo.

Kupitia ukurasa wake wa twitter leo, ameandika

“Sitashangaa. Wanatabirika. Sasa wanapaswa wasitabirike. Watumie diplomasia. Tanzania inazalisha Mahindi karibu Tani 7M (milioni) kwa mwaka.

“Kenya ni soko kubwa lazima tuendelee kulishika. Mwaka 2017 Bei ya mahindi kwa kilo ilifika shs 100 wakati sasa sababu ya Kenya ni shs 400.”

Hata hivyo, Bashe amesema hatua ya kuzuiwa mahindi. hayo, inalenga kuharibu taswira ya kilimo Tanzania, kwa kuwa Serikali ya Kenya kama ilibaini changamoto hiyo, ilipaswa kutoa hati ya malalamiko kwamba mahindi ya Tanzania yana dosari.

Mahindi yakiwa shambani

“Tanzania inapotoka zao hasa la chakula inatoa na cheti, ni utaratibu wa kidunia ambao unatambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Ni kwamba pale ambapo inakutana na tatizo kwenye zao hasa la chakula ambalo halijakidhi kiwango cha ubora wanatakiwa kutoa notice (taarifa), toka tumeanza kufanya biashara na Kenya, haijawahi kutokea tumepokea notice kama mahindi yetu yana tatizo.

“Lengo ni kuharibu taswira ya kilimo hatutaruhusu. Zao linaondoka na cheti.  Utaratibu wa kidunia ambao unatambulika na WHO duniani kote,  pale nchi inapokutana na tatizo kwenye zao hasa  chakula wanatakiwa ku-rise noncomplice notice wanatuletea sisi.

“Toka tunaanza kufanya biashara na Kenya hatujawahi kuletewa malalamiko kutoka Kenya kwamba mahindi yetu yana shida,” amesema Bashe.

Amesema, wizara yake haitaruhusu maslahi ya wakulima wa Tanzania kuharibiwa.

“Sisi Wizara ya Kilimo tumepewa jukumu na Rais John Magufuli kulinda masilahi ya Watanzania, hatutaruhusu mtu yoyote kuharibu sekta ya kilimo,” amesema Bashe.

Tangu jana Jumamosi, wafanyabiashara wa Tanzania wamezuiwa kuingiza mahindi nchini Kenya.

error: Content is protected !!