BAADHI ya viongozi na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameanza kuwasili maeneo ya Buguruni Sheli jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kushiriki maandamano yanayotarajiwa kuongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Licha ya mvua kunyesha hapa na pale, leo tarehe 24 Januari 2024, wanachama hao wa Chadema walianza kuwasili katika eneo hilo kuanzia majira ya saa 12 asubuhi, ambapo maandamano yanatarajiwa kuanza rasmi saa 3.00 asubuhi.
Hadi sasa viongozi wa Chadema waliofika katika eneo hilo ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema, Mzee Hashim Juma na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Joseph Mbilinyi (Sugu) na Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila
Akizungumza na MwanaHALISI Online, Mzee Hashim amesema kwa sasa wanamsubiri Mbowe afike ndio waanze maandamano hayo.
Aidha, amesema magari yametumwa kwenda kuwafuata wanachama katika majimbo yao ili kuwaleta eneo la tukio.
“Kiongozi wa msafara atakuwa Mbowe na msafara wetu unaanza saa tatu kamili asubuhi,mwitikio wa watu ni mkubwa na wengine wako njiani wanakuja hapa ili tukutane kwa ajili ya kuanza msafara,” amesema Mzee Hashim.
Mzee Hashim amesema kabla maandamano hayo hayajaanza wameshaona matokeo chanya, ikiwemo wanajeshi waliotajwa kufanya usafi siku ya leo kutoonekana barabarani kitendo alichoita kwamba Serikali imeheshimu uamuzi wao wa kufanya maandamano.
Pia, amesema mafanikoo mengine ni Umoja wa Mataifa (UN), kuwa tayari kuwapokea.
Kwa upande wake Sugu amesema anatarajia watanzania watatoka majumbani kwenda kujumuika nao.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema Arusha, Emma Kimambo, amesema maandamano hayo yatasaidia kufikisha malalamiko ya wananchi Kwa Serikali hasa ugumu wa maisha.
Leave a comment