Thursday , 2 May 2024
Home Kitengo Maisha Elimu CBE kuanza kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao
Elimu

CBE kuanza kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao

Spread the love

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimewataka walimu na wafanyakazi wa chuo hicho kuboresha huduma kwa wateja na kujiandaa kutoa mafunzo kidijitali ili kuendana na ongezeko kubwa la wanafunzi linalokua mwaka hadi mwaka. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, wakati akizungumza kwenye kuhitimisha wiki ya huduma kwa wateja chuoni hapo.

Alisema mwaka wa masomo ulioisha walidahili wanafunzi  6,159 kwa Kampasi ya Dar es Salaam lakini kwa mwaka huu wa masomo, kampasi hiyo  imefanikiwa kudahili kufikia 15,000.

Profesa Edda alisema kwa Kampasi za Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa imeongezeka wamedahiliwa jumla ya wanafunzi 23, 281

Alisema kutokana na ongezeko hilo la wanafunzi, walimu wa chuo hicho wanawajibika kuboresha huduma wanazotoa kwa kiwango cha juu ili kuendana na ongezeko hilo la wanafunzi.

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara, Profesa Edda Lwoga akikata keki kuwalisha wafanyakazi wa chuo hicho wakati wa kuhitimisha wiki ya huduma kwa wateja katika hafla iliyofanyika chuoni hapo.

“Hii inamaana kama ulikuwa unafundisha wanafunzi 200, idadi inaweza kuongezeka ukawa unafundisha wanafunzi 400, kila program sasa hivi tukiangalia imejaa wanafunzi kwa mfano program ya Metrology ambayo mwaka jana tulidahili wanafunzi 40 mwaka huu tumedahili wanafunzi 200,” alisema

Alisema chuo hicho kimeendelea kupanuka na kuipongeza Idara ya Masoko kutokana na jitihada kubwa wanazofanya kutangaza program za chuo.

Alisema mbali na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi, chuo hicho kimeendelea kupanua miundombinu yake kwa kujenga jingo la orofa 10 lenye thamani ya shilingi bilioni 22.4.

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara, Profesa Edda Lwoga akiwasili wakati wa kuhitimisha wiki ya huduma kwa wateja katika hafla iliyofanyika chuoni hapo.

Profesa Edda alisema jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 4,200 na aliwataka watumishi wa chuo hicho kuboresha huduma ili ziendane na ongezeko la wanafunzi.

“Tujitahidi kuanza kutoa elimu kwa njia ya mtandao, walimu wanaofundisha program za uzamili na Post Graduate mjiandae kufundisha kidijitali kwenye upande wa Utawala, Rasilimali Watu, Masoko, Biashara Kimataifa na Usimamizi wa Biashara, “ alisema

Profesa Edda alisema chuo kinapaswa kujiandaa kuhudumia ongezeko la wanafunzi kutoka nje ya nchi kwani wamekuwa wakipata wanafunzi kutoka nchi za Comoro, Congo DRC na mataifa mengine Afrika.

Alisema mbali na kutoa huduma bora kwa wateja, wafanyakazi wa chuo hicho wanatakiwa kutoa huduma bora wanapohudumiana wenyewe kwa wenyewe kwa kuhakikisha hakuna malalamiko.

Wafanyakazi wa Chuo cha Elimu ya Biashara CBE wakimsikiliza Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga wakati wa kuhitimisha wiki ya huduma kwa wateja chuoni hapo

“Sitapenda kusikia malalamiko ya wafanyakazi kwamba nimeenda kwa mtumishi flani faili langu halijatoka, usikae na faili la mtu kwa muda mrefu. Kabla hatujamnyooshea mwingine kidole tuanze kujiangalia kwanza je tunahudumiana ipasavyo na kwa wakati?” alihoji Profesa Edda.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emmanuel Munishi, alisema CBE imekuwa ikisherehekea wiki ya huduma kwa mteja kwa mwaka wa pili sasa ambapo amekuwa wakikutana na kufanya tafakari kuangalia walikotoka, walipo na wanapoelekea.

Alisema lengo la kutafakari ni kuangalia pale ambapo wamefanya vibaya na kufanya maboresho na kuenzi yale mazuri ambayo wamekuwa wakiyafanya kwenye kuhudumia wateja wao.

Alisema kwa mwaka wa masomo uliopita chuo kilifanya vizuri kwenye maeneo tafiti, kufundisha na kutoa ushauri wa kitaalalamu na kwamba idadi ya machapisho yanayotolewa na wataalamu wa chuo hicho imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Alisema huduma kwa wateja inapaswa kuwa kipaumbele namba moja na kuwataka wale ambao wamekuwa wakifanyakazi kwa mazoea kubadilika.

“Tunaomba tuboreshe mawasiliano ya sisi kwa sisi kwasababu huduma kwa wateja ni pamoja na sisi wenyewe. Mtu ukipewa kazi ukashindwa kuikamilisha toa taarifa kwamba nimefanya mpaka hapa na ukifanya vizuri ukamaliza toa taarifa pia kwamba nimekamilisha,” alisema

“Kama wewe ni mhasibu unajua unatakiwa kufanya malipo unakuta idara haina fedha badala ya kuutarifu uongozi wewe unakaa kimya, mtu wa admission na registration ya wanafunzi unakuta mfumo haufanyi vizuri umekaa kimya na wale wanaosubiri kuhudumiwa wanaendelea kuhangaika,” alisema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

ElimuHabari Mchanganyiko

Ugawaji taulo za kike watajwa kutokomeza utoro shuleni

Spread the loveBAADHI ya wanafunzi na walimu wa shule za sekondari mkoani...

ElimuHabari za Siasa

MbungeCCM ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the love  MBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze...

ElimuHabari za Siasa

Walimu 52,551 kupandishwa madaraja mwaka huu

Spread the loveNaibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala...

BiasharaElimu

NMB yatoa vifaa vya ujenzi kwa shule sita Nyasa  

Spread the loveBENKI ya NMB imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya ujenzi...

error: Content is protected !!