Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bunge laridhia itifaki kufungua soko la biashara SADC
Habari za Siasa

Bunge laridhia itifaki kufungua soko la biashara SADC

SADC
Spread the love

BUNGE la Tanzania, limeridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya 2012, yenye lengo la kufungua soko la pamoja, kuondoa vikwazo sambamba na kuelegeza masharti katika  nchi wanachama. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Itifaki hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, imeridhiwa leo Alhamisi, tarehe 31 Agosti 2023, bungeni jijini Dodoma.

Wakati akiwasilisha hoja ya kuomba Bunge kuridhia itifaki hiyo, Dk. Kijaji alitaja lengo lake ni kuimarisha SADC katika utengamano wa kibiashara na uchumi. Kwa nchi wanachama kuendelea kufunguliana fursa za kibiashara, kuondoa upendeleo, kuweka mfumo mzuri wa biashara huria na kuunda soko la pamoja.

“Lengo lingine ni kukuza ukuaji uchumi na maendeleo endelevu na kuinua viwango vya ubora wa maisha ya watu na kupunguza umaskini. Kuvutia uwekezaji kutoka nje na kuharakisha maendeleo ya wananchi wanachama kupitia sekta ya huduma,” amesema Dk. Kijaji.

Amesema sekta sita zimechaguliwa kuingia katika utekelezaji wa itifaki hiyo, ikiwemo ya mawasiliano, fedha, utalii, uchukuzi, nishati na ujenzi. Huku sekta nyingine sita zikiwa bado zinaendelea kujadiliwa ili kujumuishwa, ambazo ni pamoja na elimu, mazingira, afya ya jamii, burudani, utamaduni na michezo.

Waziri huyo wa biashara, ametaja manufaa ambayo Tanzania itayapata baada ya kuridhia itifaki, miongoni mwake ni kupatikana kwa soko kubwa la bidhaa za huduma lenye watu zaidi ya 360, kuongezeka kwa tija na ubora wa bidhaa na huduma za Tanzania kutokana na kuongezeka kwa ushindani.

Manufaa mengine ni kupungua kwa gharama za kupata huduma, upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali na uhuishaji wa teknolojia kutoka nje ya nchi kutokana na uwekezaji utakaofanyika nchini.

Baada ya Dk. Kijaji kuwasilisha pendekezo la itifaki hiyo, baadhi ya wabunge wakati wakichangia hoja, waliitaka Serikali kuendelea kuwaanda Watanzania katika kuingia kwenye ushindani pindi soko hilo litakapofunguliwa.

Mbunge Viti Maalum, Kunti Majala, alishauri Serikali iondoe changamoto za kikodi, ili kuhakikisha wafanyabiashara wa ndani wananufaika na fursa hiyo.

“Tuandae rasilimali watu yenye ujuzi, tusipoandaa masuala ya uwepo wa ajira itakuwa ndoto sababu zitachukuliwa na wenzetu. Kwa hivyo lazima tuandae rasilimali watu ambao wana ujuzi ili tukashindane tuzibebe ajira nyingi,” amesema Majala.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, alisema “ushauri wangu jambo la kwanza Serikali kwenda na muda, jambo la pili kuwaandaa watanzania ili waweze kuwahi fursa zitakazopatikana.”

Kwa upande wake Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, alishauri Sera ya nchi kuhusu mambo ya nje (diplomasia ya kiuchumi) iimarishwe ili Tanzania iweze kunufaika na maeneo mengine ya kiuchumi ambayo haijaanza kuyatumia vizuri.

Kutokana na maoni hayo, wizara ya viwanda iliwahakikishia wabunge kuwa, Serikali imeandaa mikakakti mizuri ya kuhakikisha watanzania wananufaika na soko hilo, kabla ya kuridhia itifaki.

“Moja ya sababu tumechukua muda mrefu kuridhia, ilikuwa kuwaandaa watanzania ili tunapoingia waweze kunufaika kwa asilimia kubwa na kuingia kwetu kwenye utekelezaji wa itifaki hii. Serikali yetu baada ya Rais Kikwete kusaini 2012, tulitafuta mshauri mwelekezi ambaye akazunguka katika sekta zote akakaa na wafanyabiashara wetu na tumeona tunaweza,” amesema Dk. Kijaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!