Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bodi NCCR Mageuzi yakwaa kisiki mahakamani
Habari za Siasa

Bodi NCCR Mageuzi yakwaa kisiki mahakamani

Aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani). Kulia ni aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini, Mohamedi Tibanyendera.
Spread the love

MAHAKAMA Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, imeyaondoa maombi Na. 459/2022 yaliyofunguliwa na wanaodai kuwa wajumbe wapya wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha NCCR-Mageuzi, kutokana na dosari za kisheria baada  kumfungulia shauri mtu aliyefariki dunia. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne, tarehe 13 Desemba 2022 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Ephery Kisanya, baada ya mawakili wa waleta maombi kuomba kuyaondoa kufuatia kumfungulia shauri mtu aliyefariki dunia.

Jaji Kisanya ameyaondoa maombi hayo mahakamani  bila masharti ya gharama kutokana na waleta maombi kudai kuwa hawakuwa na taarifa kwamba mjibu maombi huyo namba tano amefariki dunia.

Hata hivyo, Jaji Kisanya ametoa nafasi kwa upande wowote utakaotaka kufungua kesi hiyo iliyolenga kuhoji uhalali wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha NCCR-Mageuzi, kuyaleta upya.

Awali, Wakili wa waleta maombi, Novatus Muhangwa, aliiomba mahakama hiyo iyaondoe maombi waliyowasilisha kupinga wajumbe wa zamani wa bodi hiyo ambao wamefungua kesi ya msingi Na. 150/2022 kupinga kung’olewa madarakani kwa waliokuwa viongozi wa chama hicho, akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti, James Mbatia.

Maombi hayo yalifunguliwa na Beati Mpitabakama na wenzake dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mohamed Tibanyendera.

Wakili Muhangwa alitoa maombi hayo, baada ya mawakili wa wajibu maombi wakiongozwa na Wakili Hudson Mchau, kuweka lingamizi dhidi ya maombi yao ya kutaka kumuondoa katika orodha ya wajibu maombi, marehemu Rakia Abubakar, ambaye alikuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini ya NCCR-Mageuzi.

Kwa mujibu wa Wakili Mchau, kesi hiyo haikustahili kuwepo mahakamani kwa kuwa miongoni mwa walioshtakiwa alifariki Dunia tarehe 30 Januari 2021, kabla kesi hiyo haijafunguliwa tarehe 7 Oktoba 2022.

Akizungumza baada ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NCCR-Mageuzi, Mohamed Tibanyendera, amedai ni ishara kwamba haki itatendeka katika kesi ya msingi ambayo inaendelea kusikilizwa mahakamani hapo.

“Mliyoyasikia ndiyo yamejiri mahakamani, chama kiko imara na bodi iko imara na tunaamini misukosuko itaisha. Kilichoendelea kuhusu uamuzi wa kuteua wajumbe wa bodi ya wadhamini ya Mpitabakama yaliazimia kuondoa wajumbe halali,” amedai Tibanyendera na kuongoza:

“Sasa unapomuondoa marehemu kwenye uongozi na hunawahi msikiliza inakuwaje? Hiyo ndiyo hoja iliyokuwepo mahakamani tunashtaki sababu tunaamini tulinyimwa haki ya kusikilizwa.”

Tibanyendera na wenzake, walifungua kesi ya msingi kupinga uamuzi wa chama hicho kuwaondoa madarakani waliokuwa viongozi wa NCCR-Mageuzi pamoja na kuvunja sekratarieti yake ya uongozi.

Katika kesi hiyo, Tibanyendera na wenzake wanadai vikao vilivyomuondoa Mbatia na wenzake, vilikuwa sio halali.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!