Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Sabaya aweka pingamizi rufaa ya Jamhuri
Habari za SiasaTangulizi

Sabaya aweka pingamizi rufaa ya Jamhuri

Spread the love

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha kesho tarehe 14 Disemba, 2022 inatarajiwa kutoa uamuzi mdogo juu ya mapingamizi mawili yaliyowasilishwa na mawakili wa aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake watano kupinga rufaa iliyokatwa na upande wa Jamhuri dhidi ya Hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, iliyowaachia huru. Anaripoti Grace Macha, Arusha …. (endele).

Tarehe 10 Juni, 2022 Sabaya na wenzake sita walishinda kesi ya uhujumu uchumi na kuachiwa huru baada ya mahakama hiyo kubaini ushahidi uliotolewa na Jamhuri ulighubikwa na utata hivyo kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yanawakabili na kuwatia hatiani.

Mawakili hao wa upande wa Sabaya wameweka mapingamizi hayo wakidai maombi hayo ya rufaa yamewasilishwa mahakamani nje ya muda na majina ya wajibu rufaa yaliyo kwenye kusudio la kukata rufaa ya Juni 24, mwaka huu  yanapishana na yale yaliyo kwenye rufaa iliyowasilishwa mahakamani hapo Oktoba 28, mwaka huu.

Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza maombi hayo ya rufaa namba  155/2022 amepanga kutoa uamuzi huo kesho saa tatu asubuhi baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili.

“Notisi ya kukata rufaa ilikuwa ya watu saba, ikiwemo mjibu rufani namba tatu Watson Mwahomange, ila kwenye maombi ya rufaa yaliyowasilishwa mahakamani mjibu rufani huyo wa tatu hayupo hivyo kufanya rufaa kuwa na watu sita badala ya saba kama ilivyo kwenye notisi ya kukata rufaa,” alieleza Wakili wa Sabaya, Moses Mahuna na kuongeza.

“Tunafahamu kifungu cha 386(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai DPP anaweza wakati wowote kabla ya kusililizwa kwa shauri kuondoa hati ya rufaa kwa kuandika notisi kwa msajili wa mahakama kuu dhidi ya mtu fulani au kuondoa rufaa yote.

“Hii imekuja kusikilizwa leo hatujawahi kuona notisi ya msajili inayoondoa hiyo kesi dhidi ya Watson na kutuambia sasa rufaa hii itabaki na watu sita hivyo ni wasilisho letu kwamba notisi ya rufaa ambayo ndo ilileta rufaa inatofautiana na maombi yaliyopo hapa,” alisema.

Upande wa Jamhuri unawakilishwa na jopo la mawakili wa serikali waandamizi watano, Patrick Mwita, Abdallah Chavula, Hebel Kihaka, Felix Kwetukia na Timotheo Mmari.

Lengai Ole Sabaya akiwa mahakamani Arusha

Wakijibu hoja hizo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwita alieleza kuwa taratibu zote za kisheria zimefuatwa ikiwemo kuwasilisha kusudio la kukata rufaa na rufaa yenyewe ndani ya muda wa siku 45 tokea wapatiwe nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi.

Pingamizi lao limeegemea sehemu ndogo ya sheria wametafsiri sheria kwamba kuanzia siku hukumu inasomwa Juni 10, mwaka huu mpaka muda wa kuwasilisha rufaa Oktoba 28, mwaka huu.

“Tafsiri ya wakili Mahuna kwamba huu muda unaanza kuhesabiwa mara baada ya hukumu amekosea hii inaanza kuhesabiwa baada ya kupata nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi,” alieleza wakili wa serikali Mwita huku akisisitiza kuwa sababu yao ya kwanza ya pingwmizi la awali haina msingi hivyo itupiliwe mbali

Akijibu hoja yao ya pili ya kuwa kusudio la kukata rufaa walilowasilisha  mahakamani Juni 24,  mwaka huu ina wajibu rufaa saba lakini maombi ya rufaa  yaliyowasilishwa Oktoba 28, mwaka huu yana wajibu rufaa sita.

“Napenda mahakama izingatie lugha anayotumia Wakili Msomi Mahuna  ni hatari kwani jamii inaweza kuamini kuwa ndivyo kumbe sivyo. Anasema ‘notice of appeal’ ina watu tofauti kabisa na wale waliokatiwa rufaa,” alieleza wakili wa serikali Mwita na kuongeza.

“Inatia ukakasi kabisa kwenye uwakili hiyo si sawa kabisa. Kwenye rufaa anasomeka Enock Togolan Mkeni ambapo notisi ya kukata rufaa ni Watson Mwahomange ambaye tuna sababu za kutomweka tutazieleza baadaye,”

“Kwenye nia ya kukata rufaa tuliwaweka waliokuwa washitakiwa  wote saba. Ndani ya siku 30 baada ya hukumu kusomwa hii inaanzisha rufaa hivyo maombi ya rufaa huwasilishwa baada ya kupata hukumu na mwenendo wa shauri na kujua ‘strength’ ya shauri lako na ndipo unapoandaa hoja za rufaa.

“Upande wa rufaa baada ya kuona hukumu tukaona hatuna haja ya kuendelea na Watson Mwahomange. Kifungu cha 386 cha CPA alichotumia Mahuna kusema kuwa upande wa waleta rufaa walipaswa kukitumia kuieleza mahakama kuwa wanamtoa mwahomange haiko sawa.

“Hatutajua kutokuwepo kwa Watson Mwahomange kunaathiri vipi haki ya wajibu rufaa na sisi ndiyo tunaoamua tunakata rufaa kwa ajili ya nini na nani hatupangiwi,” amedai.

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Chavula aliomba mapingamizi hayo ya awali yatupwe kwa kile alichoeleza kuwa pingamizi la awali linapaswa kuwekwa kwenye masuala ya kisheria na si ya kiuchunguzi kama mawakili wa  wajibu rufaa walivyofanya.

“Ni mtizamo wetu kwamba hoja za wenzetu za kukiukwa kifungu cha  379 kifungu kidogo cha kwanza b cha CPA kilichofanyiwa marekebisho  2022 kuhusiana na muda wa kufunguliwa kwa rufaa ni hoja ambayo si ya kisheria kwani inahitaji uthibitisho. Mahakama inahitaji ichunguze nyaraka na walioleta hoja hii wanatakiwa waipatie mahakama nayaraka hizo,” alieleza Chavula na kuongeza.

“Hoja hii inatoka ‘bar’ kwenda ‘bench’ ni msimamo wa kisheria kuwa mapingamizi ya awali ni lazima yajielekeze kwenye hoja za kisheria na si kiuchunguzi,’.

Chavula alirejea maamuzi  yaliyowahi kufanywa na mahakama ya rufaa huku akisisitiza kuwa kutokana na msingi huo pingamizi hilo halikidhi vigezo vya kisheria la kuwa sababu ya pingamizi la awali la rufaa.

Mbali na Sabaya wajibu rufaa wengine ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya ambapo wajibu rufaa waliokuwa mahakamani ni Sabaya na Nyegu.

Tarehe 10 Juni, 2022, Hakimu Patricia Kisinda aliwaachia huru Sabaya na wenzake sita katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2022 na kudai kuwa ushahidi uliotolewa na Jamhuri uligubikwa na utata, hivyo kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yanawakabili na kuwatia hatiani.

Aidha, tarehe 6 Mei, 2022  Sabaya na wenzake wawili Nyegu na Daniel Mbura, walishinda rufaa iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, waliyokata kupinga hukumu ya miaka 30 iliyokuwa imetolewa na na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Kwa sasa Sabaya yupo mahabusu katika gereza la Karanga kwa kuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!