December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Bima ya afya kwa wote kuanza Julai 2023

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Spread the love

 

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema bima ya afya kwa wote itaanza kazi kuanzia tarehe 1 Julai 2023, endapo Bunge la Tanzania, litapisha muswada wa sheria yake Novemba, mwaka huu. Anaripoti Urumasalu Kisung’uda, TUDARCo … (endelea).

Ummy ametoa taarifa hiyo leo Jumanne, tarehe 27 Septemba 2022, ikiwa ni siku nne tangu Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, usomwe kwa mara ya kwanza, bungeni jijini Dodoma, tarehe 23 Septemba, mwaka huu.

Waziri huyo wa afya amesema, kabla ya bima hiyo kuanza kutumika, Serikali itatumia kipindi cha miezi sita, kupata utaratibu wake, ikiwemo vifurushi.

“Katika Bunge la Novemba, utasomwa mara ya pili, ukipita Novemba tutaanza kutekeleza kuanzia tarehe 1 Julai 2023. Jambo hili wabunge walilitaka kwa muda mrefu, ni jambo linalowezekana kupita. Miezi sita itatumika kuweka utaratibu wa vifurushi,” amesema Ummy.

Akielezea mapendekezo ya muswada wa bima hiyo, Ummy amesema wamependekeza mwananchi kulipia gharama za vifurushi kwa awamu, kuanzia miezi mitatu hadi minne kwa mwaka, huku akisema wasiokuwa na uwezo Serikali itaanzisha utaratibu wa kuwatambua na kuwaunganisha katika bima hiyo.

“Kwenye hii bima utachagua bima yako, unaweza kukata ya binafsi au ya Serikali, suala ni kwamba upate bima ya afya. Kwenye muswada huu tunapendekeza kuweka kitita cha mafao chenye usawa ambacho kila mwananchi atakayejiunga na bima atakuwa na haki ya kukipata. Tutakuja na viwango mbalimbali mtu kujipimia,” amesema Ummy.

Ummy amesema, Serikali imependekeza wananchi watakaojiunga na bima hiyo, kupata vipimo muhimu vya maabara kama, X-Ray, CT Scan na Ultra Sound.

Amesema, bima ya afya kwa wote ni lazima lakini wananchi wasiojiunga nayo hawatachukuliwa hatua za kisheria, huku akisema  ili kuhakikisha wananchi wengi wanajiunga na bima hiyo, Serikali imependekeza kufungamanisha huduma hiyo na baadhi ya huduma za umma, kama leseni ya biashara na udereva.

“Hakuna mtu atakamatwa, atafungwa au atalipishwa faini kwa kutokuwa na bima ya afya, hakuna hicho kifungu. Lakini tunawapataje Watanzania ambao hawaumwi wajiunge na bima, ndiyo maana tumependekeza kuifungamanisha na baadhi ya huduma, tunasema unataka leseni ya biashara, udereva, kitambulisho cha NIDA, bima ya afya iko wapi,”amesema Ummy.

Ummy amesema Serikali inakusudia kuanzisha bima hiyo ili kumsaidia mwananchi kumudu gharama za matibabu, hata katika kipindi ambacho hana fedha.

“Tumeona watu wengi wanatumia fedha nyingi kulipia huduma za matibabu, sasa utaratibu wa malipo ya papo kwa papo imekuwa changamoto kubwa inayosababisha wananchi wengi kutopata uhakika wa kupata huduma za afya pindi wanapougua,” amesema Ummy.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga

Ummy amesema “tumekuta wananchi wanauza mashamba yao, pikipiki, wengine mpaka nyumba wakiwa wagonjwa ili kupata huduma za afya. Kwa mfano sasa hivi kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo matibabu yake ugharimu fedha nyingi,”

“Mathalani gharama ya tiba ya Saratani ni kama Sh. 26 milioni kwa mwaka. Gharama ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo ni Sh. 32 milioni kwa mwaka. Wananchi wengi wanashindwa kumudu na kupata athari zaidi za kiafya na wengine kupoteza maisha.”

Waziri huyo wa afya amesema kwa sasa asilimia nane tu ya Watanzania ndiyo wenye uhakika wa kupata huduma za afya, kwani wamejiunga na bima za afya kubwa, huku asilimia saba wakiwa wamejiunga bima za afya za kawaida.

Amesema, asilimia 15 kati ya watanzania milioni 60, ndiyo waliojiunga na bima za afya.

error: Content is protected !!