December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wataka mjadala kupata mwarobaini  ukata vyombo vya habari

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben

Spread the love

 

WADAU wa tasnia ya habari, wameshauri uitishwe mjadala wa kitaifa, kujadili namna ya kutatua changamoto ya kifedha katika vyombo vya habari. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ushauri huo umetolewa kwa nyakati tofauti na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari, wakitoa mapendekezo yao juu ya namna ya kuimarisha uchumi wa vyombo vya habari, ili vijiendeshe kwa uhuru pamoja na kulipa stahiki za wafanyakazi wake.

Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Reuben, amesema mjadala huo utasaidia kuangalia namna ya kuboresha mifumo mipya uendeshaji vyombo hivyo, badala ya kutumia mifumo ya kizamani ambayo imepitwa na wakati.

“Uchumi wa vyombo vya habari ni mjadala mzito ambao upo, kwa sababu vyombo hivi ambavyo inakuwa vimeanzishwa vingine ni vya watu binafsi, mashirika ya serikali na taasisi mbalimbali. Tunajua ya kwamba rasilimali za uchumi hasa fedha imekuwa tatizo nadhani kama taifa tuweke mijadala kwa sababu wenzetu huko nje taarifa za habari zinauzwa,” amesema Rose na kuongeza:

“Kama nje, taarifa hizi zinauzwa ili kazi ya mwandishi wa habari zisitumike bure, itumike kama sehemu ya kujipatia kipato lakini pia wenye vyombo watafute namna ya kuweza kupata mapato ambayo yatawezesha kuwapatia taarifa mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya umma wetu. Na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi za kitaifa na kimataifa wanapaswa kupeleka matangazo ama kulipia baadhi ya huduma wanazohitaji katika vyombo vya habari.”

Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo, amevishauri vyombo vya habari kuja na muundo mpya wa kufanya biashara, badala ya kutegemea mauzo ya magazeti na matangazo, huku akivishauri kuandaa maudhui ya habari yanayouzika sokoni.

Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo

“Kwanza, nashauri vyombo vya habari kubadilisha muundo wa biashara zao, zibadilike na si kutegemea kuuza magazeti na matangazo tu. Pili, vyombo vianze kutengeneza maudhui yanayouzika ambayo yatawalipa mfano makala kama wafanyavyo Al-Jazeera,” amesema Nsokolo na kuongeza:

“Tatu, wawe na matumizi mazuri ya uandishi wa habari wa kidigitali (digital journalism), katika mitandao ya kijamii ambayo ina watumiaji wengi kwa sasa. Kuwa na online subscribers ambao watatakiwa kulipia kwa siku, mwezi au mwaka. Hii itawasaidia kuongeza kipato.”

Wakili wa kujitegemea, James Marenga, ameishauri Serikali ifanye marekebisho ya baadhi ya vifungu vya sheria, ambavyo kwa namna moja au nyingine vinadidimiza uchumi wa vyombo vya habari, ikiwemo kifungu cha 5 (1) cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016, kinachompa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, kuratibu matangazo pamoja na kukata asilimia 10 ya mauzo ya kila tangazo.

“Kifungu cha 5(l) cha sheria ya Huduma za Habari na kanuni ya  25 (1-5) ya kanuni za sheria ya Huduma za Habari 2017,  vinampa mamlaka makubwa mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kuratibu matangazo kutoka taasisi za umma na halmashauri. Mkurugenzi anaweza kuamua wapi apeleke matangazo hayo. Pia atakuwa anakata asilimia 10 ya mauzo ya kila tangazo,” amesema Marenga na kuongeza:

“Hatari ni kuwa, vyombo vya binafsi vinaweza kukosa matangazo kama vitaandika habari zisizo pendeza serikali. Kifungu kingine ni kifungu cha 5(i) na Kanuni ya 4(1)(a) na (b) za sheria hiyo, zinampa mamlaka ya kusajili magazeti na kusimamia umiliki wa vyombo vya habari vya magazeti,”

“Vifungu hivi vinadhoofisha vyombo vya habari, maana vinalazimika kusajili kila mwaka na pia uanzishwaji wa vyombo vya habari vya kimagazeti hautaruhusu watu wa nje ya nchi, kumiliki zaidi ya asilimia 49 hivyo kunyima wigo wa uwekezaji kwa wageni na kuendeleza vyombo vya habari kibiashara.”

Waandishi wa Habari

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Selemani Msuya, ameshauri Serikali iweke muongozo utakaowezesha vyombo vya habari kuomba matangazo moja kwa moja, kutoka katika taasisi za umma na binafsi pamoja na makampuni, badala ya kwa mawakala kama ilivyo sasa.

Msuya amesema kuwa, muongozo huo pia uzielekeze taasisi na kampuni hizo kuwa na bei elekezi za matangazo kwa vyombo vya habari vyote, badala ya ilivyo sasa bei zinatofautiana kulingana na ukubwa au hadhi ya chombo husika.

Katika hatua nyingine, Msuya ameishauri Serikali kuweka takwa la kisheria kwa watu wanaotaka kusajili vyombo vya habari, kuwa na mpango mkakati unaonesha namna watakavyojiendesha ikiwemo vyanzo vya mapato, ili kuepusha utitiri wa vyombo vya habari ambavyo haviwezi kujiendesha.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Idara ya Habari Maelezo, magazeti na majarida yaliyosajiliwa ni 257, wakati vituo vya redio vilivyosajiliwa ni 210, televisheni (56), redio za mtandaoni (24), televisheni za mtandaoni (663), tovuti na mitandao ya habari zaidi ya 200.

Mdau mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina, ameshauri Serikali iweke vifungu vya sheria vinavyoimarisha uhuru wa vyombo vya habari kuandika habari za uchunguzi, ili viweze kuvutia wasomaji na watazamaji wengi kwa ajili ya kupata kipato.

“Tanzania tuna watu takribani milioni 60, lakini gazeti linaloongoza kuuza sokoni linachapisha nakala 10,000 na zingine zinabaki. Hii inaonesha kuwa watu hawanunui magazeti, angalu kampuni za magazeti zingeuza nakala kuanzia 100,000, wangepata faida,” amesema.

error: Content is protected !!