August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ajiteketeza kwa moto kisa mateso ya Wachina

Spread the love

S. Erdene, kiongozi wa chama cha wafanyakazi wa migodi nchini Mongolia amejichoma moto akishinikiza serikali kuachana na mikataba ya kibiashara na makampuni kutoka China, anaandika Wolfram Mwalongo.

Picha ya video inayopatikana hivi karibuni ikionesha tukio hilo imewashtua wengi ingawa tukio lilitokea mwishoni mwa mwaka jana akiishutumu serikali ya Mongolia kufumbia macho mikataba ya kinyonyaji kutoka makampuni ya wachina.

Erdene aliitisha mkutano na wanahabari ili kujadili mabadiliko ya mikataba kwa wafanyakazi wa mgodi wa TaivanTolgoi unaosifika ulimwenguni kwa uzalishaji mkubwa wa Makaa ya mawe unaomilikiwa na kampuni kutoka China.

Kabla ya kuchukua uamuzi huo Erdene aliishutumu nchi yake kwa kile alichodai inauza raia wake kwa mataifa ya kigeni na kwamba kama serikali inataka kuwateketeza raia wake ni bora wajichome moto wenyewe kuliko manyanyaso kutoka kwenye kampuni za kigeni ndani ya nchi yao.

Baada ya maneno hayo kiongozi huyo wa wafanyakazi alitoa kifaa kutoka mfukoni mwake kinachoaminika kuwa ni kiberiti na kujiwasha moto hata hivyo mashuhuda waliuzima moto huo huku ukiwa umemjeruhi kwa kiasi.

https://www.youtube.com/watch?v=svLLETzXcLo

Kampuni ya Tavan Tolgoi inatuhumiwa kuhamishia mikataba ya wafanyakazi zaidi ya 200 kwenye makamuni ya kichina jambo ambalo wafanyakazi hao hawakuliafiki.

Wafanyakazi hao wamekuwa wakitumikishwa kazi ngumu na nyingi kinyume na mikataba yao huku pia vitendo vya unyanyasaji vikiripotiwa.

Inakadiriwa kuwa asilimia zaidi ya 86 ya mauzo ya madini ya Mongolia huuzwa nchini China, Ambapo China pia huuza katika mataifa mengie ya Magharibi na America huku uchumi wa Mongolia ukizidi kuzorota kila uchao.