December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Afghanistan hali tete Taliba ikichukua nchi, rais akimbia

Spread the love

 

SERIKALI ya Afghanistan iko katika wakati mgumu baada ya Rais wake, Ashraf Ghani, kukimbia kufuatia hatua ya kundi la wanamgambo wa Taliban, kuiteka nchi hiyo. Inaripoti mitandao ya kimataifa … (endelea).

Taarifa ya Rais Ghani na makamu wake wa rais, Amrullah Saleh, kukimbia nchi, imtolewa jana tarehe 15 Agosti 2021, saa chache baada ya kundi hilo kuteka Ikulu iliyopo katika Mji wa Kabul.

Rais huyo anadaiwa kuchukua hatua hiyo , akikwepa kujisalimisha kwa wanamgambo wa Taliban.

Pia, wananchi wa Taifa hilo ikiwemo raia wa kigeni, tangu jana wameanza kukimbia nchi hiyo, wakikwepa utawala wa Taliban, unaodaiwa kuwa wa itikadi kali za kiislamu.

Wakati raia wakijaribu kuyakimbia makazi yao, mataifa takribani 60 yamehimiza wananchi hao waruhusiwe kuondoka kwa amani nchini humo.

Nchi ya Marekani na mataifa ya magharibi, yameanza kuwaondoa raia wake, wakiwemo wanajeshi na wanadiplomasia.

Hadi sasa, watu watano wamefariki dunia katika Uwanja wa Ndege wa Kabul nchini humo, wakigombania kupanda ndege kwa ajili ya kwenda nchi jirani.

Mbali na kuiteka Ikulu, wanamgambo wa Taliban wamechukua miji muhimu, ukiwemo wa Mazar-i-Sharif, ambao ni makao makuu ya Serikali ya Afghanstan.

Hadi leo Jumatatu, Taliban imefanikiwa kudhibiti majimbo 23, kati ya 34 nchini humo.

Msemaji wa Taliban, Mohammad Naeem, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba, vita imeisha baada ya kundi hilo kufanikiwa kuiteka nchi.

Naeem amesema kuwa, kundi hilo limepata kile ilichokitaka kwa muda mrefu, kuliongoza Taifa lao kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mataifa ya nje.

Mitandao ya kimataifa imeripoti kuwa, Taliban wameanza harakati za kuunda Serikali yao na kwa sasa wameanza kupeana uongozi katika majimbo ya nchi hiyo.

Kundi hilo linamenukuliwa likisema, linasubiri wanajeshi wa kigeni kuondoka nchini humo, ili liunde Serikali kamili.

Kwa sasa kundi hilo limewaruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao.

error: Content is protected !!