Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ACT-Wazalendo yalaani mauji operesheni za jeshi la polisi
Habari za SiasaTangulizi

ACT-Wazalendo yalaani mauji operesheni za jeshi la polisi

Mbarara Maharagande, Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu na Makundi Maalumu ya Chama cha ACT-Wazalendo
Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeelaani  vikali kile kilichodai ni ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini Tanzania katika operesheni zake zinazoendelea za kuzuia uhalifu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Kimesema licha ya kupokea kwa faraja mwitikio wa jeshi hilo katika kushughulikia matukio ya uhalifu na hatua ya kusambaratisha mtandao wa uhalifu, lakini utekelezaji wake “kukiuka haki za binadamu na kupuuza matuamizi ya weledi, utawala wa sheria na kulinda haki za wananchi.”

Hayo yameelezwa leo Jumanne tarehe 4 Oktoba, 2022 na Msemaji wa Sekta ya Mambo ya Ndani ya Nchi wa ACT-Wazalendo, Mbarala Maharagande, katika mkutanoi wake na waandishi wa Habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Maharagande amesema kinyume na matarajio yao utekelezaji wa Operesheni hizo zimeibua hofu, wasiwasi na kuvuruga amani ya wananchi.

“Hadi sasa kuna mamia ya vijana wanaotuhumiwa na matukio hayo ya kihalifu wameripotiwa kukamatwa. Matukio yaliyotushtusha zaidi ni taarifa za mauaji ya watu sita jijini Dar es Salaam yaliyothibitishwa na Jeshi la Polisi lenyewe kupitia vyombo vya habari Tarehe 18 Septemba 2022,” amesema Maharagande.

Jeshi la Polisi katika taarifa yake kuhusu mauji hayo lilisema watuhumiwa walijeruhiwa wakati wakijaribu kutoroka baada ya kukataa amri ya kujisalimisha na kufariki wakati wakipelekwa hospitalini.

Amesema kuwa Polisi walithibitisha kuua watu watatu huko Serengeti, Mkoa wa Mara Tarehe 21, Septemba 2022.

Polisi ilisema watuhumiwa walijeruhiwa baada ya majibizano ya risasi na wahalifu wenzao ambao waliwapeleka kuonyesha walipoficha silaha zao lakini wakavamiwa huku wao wakijaribu kutoroka.

“Mauaji haya, yalianza kuwashtua wadau na wanaharakati na kuacha maswali namna Polisi wanavyoendesha Operesheni zake. Ikiwa polisi wanajipa haki za kukamata, kuhukumu na kutoa adhabu tena adhabu za kifo kwa watuhumiwa ni dhahiri tunaruhusu mfumo wa utendaji usiozingatia haki na mgawanyo wa majukumu, ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu,” amesema Maharagande.

Ameongeza kuwa pamoja na kuwepo na taarifa za mauaji ya watuhumiwa wa uhalifu ambazo Polisi wenyewe wamekiri hadharani lakini polisi hawatangazi kila tukio la mauaji linalofanywa na wao katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine.

Kutokana na hali hiyo chama hicho kimelitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liunde Tume ya kuchunguza mauaji yote ya raia ili kujiridhisha na hatua zilizofanywa na Jeshi la Polisi na kuwataka maafisa wa Jeshi la Polisi wanaotuhumiwa na mauaji kusimamishwa ili kupisha uchunguzi.

Pia kimemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kujiuzulu mara moja kutokana na kushindwa kuchukua hatua tangu matukio haya yaliporipotiwa na maofisa wote wanaohusika na mauaji hayo wachukuliwe hatua.

“Ni jambo la kusikitisha wakati nchini kote kukiwa na hitajio kubwa la mageuzi ya utendaji na uendeshaji wa Jeshi la Polisi kuona askari Polisi wanaendelea kufanya matukio yanaongeza hasira, mashaka na kujenga uhasama baina ya Jeshi hilo na wananchi, » amesema.

Katika hatua nyingine chama hicho kimesema kinapinga « njama na hila hizi za kisiasa » zinazofanywa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Tunduru kufuatiwa Katibu Mkuu wake Ado Shahibu kukataliwa kufanya mikutano ya hadhara mkoni Mtwara kwa kile kilichoelezwa ni uwepo wa matishio ya matukio ya kigaidi.

Jana Tarehe 3/10/2022 Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tunduru alikiandikia Chama barua yenye Kumb. Na. TUN/A.7/6/VOL.II/87 yenye kichwa cha Habari “KUKATALIWA KUFANYA ZIARA YA KATIBU MKUU WA ACT NDUGU ADO SHAIBU”, kutokana na sababu alizozieleza kuwa kutokana na kuwepo kwa matishio ya kigaidi.

“Hili ni jambo kubwa ambalo linahitaji mazingatio mapana; kwanza suala la uwepo wa matishio hayo lilipaswa kutolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini ambaye ndiye mwenye Wajibu wa msingi wa uratibu wa masuala hayo makubwa ambayo kutangazwa kwake kunaweza kuleta athari ya kiuchumi Kitaifa, kuathiri biashara ya Utalii na uwekezaji nchini,” amesema Maharagande na kuongeza;

“Haiwezi kuwa tishio hilo la ugaidi linakuwepo pale ACT Wazalendo inapofanya shughuli zake za kisiasa, Kikatiba ndipo lizuke tishio la ugaidi, lakini CCM na Viongozi wake wanapofanya ziara kama hizo pasiwepo na tishio la Ugaidi.

“Tunapinga vikali njama na hila hizi za Kisiasa zinazofanywa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Tunduru na Watendaji wengine wa Kiserikali ambao tunaamini tamko hilo la Jeshi la Polisi limetaratibiwa pamoja nao.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!