Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko NMB yazindua mikopo nafuu elimu ya juu, Waziri Mkenda asema…
Habari Mchanganyiko

NMB yazindua mikopo nafuu elimu ya juu, Waziri Mkenda asema…

Spread the love

BENKI ya NMB imetenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyakazi wanaotaka kupata elimu ya juu au wale wanaohitaji fedha za kuwasomesha wategemezi wao. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Bidhaa hiyo mpya ya mikopo nafuu inayoleta ahueni kubwa katika ufadhili wa hasa elimu ya juu nchini imezinduliwa rasmi leo Jumanne jijini Dodoma na tayari inapatikana kwenye matawi yote ya benki hiyo yaliyotapakaa nchi nzima.

Mkurungenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimi ya Juu, Abdul-Razaq Badru akimpongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (watatu kulia) mara baada ya uzinduzi wa mikopo ya elimu ya Juu hapa nchini inayotolewa na benki ya NMB. Benki ya NMB imetenga sh bilioni 200 kwa ajili ya mikopo hiyo kwa mwaka huu. Uzinduzi huo ulifanyika leo Jijini Dodoma, wengine katika picha kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Aldof Mkenda na wapili kulia ni Afisa Mkuu wa wateja binafsi na biashara,Filbert Mpozi mwisho ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi.

Mbali na vyuo vikuu, huduma ya ufadhili huu ambayo jina lake la kibiashara ni ‘NMB Elimu Loan’ itatolewa pia kwa ngazi zote za elimu zikiwemo shule za msingi na secondari hata vyuo vya ufundi.

Akitangaza kuanzishwa kwake rasmi leo tarehe 14 Machi 2023, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema mikopo inayotolewa kwa mwajiriwa yeyote inaanzia Sh 200,000 hadi Sh milioni 10 kwa mwaka kwa mtu mmoja.

Zaipuna amesema moja ya sifa za kupata mkopo huo, wenye riba ya asilimia tisa tu na ambao marejesho yake ni ndani ya miezi 12, ni kuwa mwajiriwa ambaye ni mteja wa NMB.

“Kuanzia leo (Jumanne), tumeanza rasmi kupokea maombi ya mkopo kwa ajili ya kugharamia elimu kwa wafanyakazi ambao mishahara yao inapita Benki ya NMB,” amesema Zaipuna.

“Huu ni utekelezaji wa makubaliano yetu na Wizara ya Elimu ya kuanza kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kupunguza utegemezi wa  waajiriwa kwa bodi ya mikopo (HESLB) pale wanapotaka kujiendeleza kimasomo na pia kuwalipia ada vijana wao,” amefafanua.

Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia ,Prof Aldof Mkenda (wanne kukhoto) akimpongeza Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) NMB ,Ruth Zaipuna (watatu toka kulia) mara baada ya NMB kuzindua rasmi wa mikopo ya elimu ya Juu itakayotolewa na benki hiyo,NMB imetenga sh bilioni 200 kwa ajili ya mikopo hiyo ya elimu ya juu nchini,wengine katika picha kutoka kushoto ni Naibu Waziri wizara hiyo,Omari Kipanga,Katibu Mkuu Wizara hiyo,Prof.Carolyne Nombo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Elimu, Utamaduni na Michezo, Prof Kitila Mkumbo na kutoka kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati ,Nsolo Mlozi na wapili ni Afisa Mkuu wa wateja binafsi na biashara, Filbert Mponzi, uzinduzi huo ulifanyikja Jijini Dodoma jana

Aidha, amesema NMB ina dhamira ya dhati katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha tasnia ya elimu na kuchangia kutoa elimu bora kwa wote huku ikiwa mstari wa mbele kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha za kuwafadhili wote wanaohitaji kujiendeleza kielimu.

“Tumezindua huduma hii hapa Dodoma leo lakini mikopo hii inatolewa katika matawi yetu yote nchi nzima,” afisa huyo amebainisha na kusema fedha zitakazotolewa zitaingizwa moja kwa moja katika akaunti ya shule au chuo husika na wala si vinginevyo.

“Ili kupata mkopo huu, fika tawi lolote la NMB na nakala ya mshahara wako, mtiriko wa ada, barua ya kujiunga na chuo na wafanyakazi wa Benki ya NMB watakupigia hesabu ya mkopo unaostahili kupata,” amesema Zaipuna.

Kwa kuanzisha huduma hii, NMB inakuwa imetimiza ahadi iliyoitoa mwaka jana yakuisaidia Serikali kuipunguzia HESLB mzigo wa kufadhili masomo ya juu na kuwa na vyanzo vipya vya mikopo ya elimu.

Mwishoni mwa mwaka 2022, benki hiyo ilifanya makubaliano na Serikali kupitia Wizara ya Elimu ya kuanza kuwakopesha wazazi kwa riba nafuu ili waweze kugharamia elimu yao ya juu au kuwasomesha wategemezi wao.

“Yote haya yanalenga kuendeleza juhudi za kukuza sekta ya elimu hapa nchini, na sisi kama wadau wakuu wa elimu, tumeona tutoe ushirikiano huu kwa serikali kwa manufaa ya watanzania wenzetu,” amesema Zaipuna huku akisisitiza kuwa NMB itaendelea kubuni suluhishi zaidi za kuboresha elimu na kuimarisha tasnia hiyo.

Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia, Prof. Aldof Mkenda (wanne kushoto) akishirikiana na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) NMB, Ruth Zaipuna (watatu toka kulia) kufungua pazia kuashiria uzinduzi rasmi wa mikopo ya elimu ya Juu inayotolewa na benki hiyo. NMB imetenga sh bilioni 200 kwa ajili ya mikopo hiyo ya elimu ya juu nchini,wengine katika picha kutoka kushoto ni Naibu Waziri wizara hiyo,Omari Kipanga, Katibu Mkuu Wizara hiyo,Prof.Carolyne Nombo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Elimu, Utamaduni na Michezo, Prof Kitila Mkumbo na kutoka kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi na wapili ni Afisa Mkuu wa wateja binafsi na biashara,Filbert Mponzi. Uzinduzi huo ulifanyika Jijini Dodoma leo.

Katika hotuba yake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda aliyekuwa mgeni rasmi ameweka bayana matamanio yake ya kutaka kupatikana ufadhili zaidi ya kile ilichokifanya NMB kutoka kwa wadu wengine.

Aidha, amesema uwekezaji wa NMB ni kitu kikubwa kinachoongeza wigo wa watu kujisomesha na akaomba hela za mikopo hiyo zitumike kwa ajili ya madhumuni yaliyokosudiwa tu.

Waziri huyo amesema pamoja na bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kuongezeka kutoka Sh bilioni 464 Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani hadi Sh bilioni 657 kwenye mwaka huu wa fedha bado kuna uhitaji wa vyanzo vingine kama hiki kipya kilichoanzishwa na NMB.

“Nikiri kuwa nyie ni wadau wa kweli wa elimu nchini na mmeonyesha njia inayostahili kuzingatiwa na wadau wengine,” Prof Mkenda amesisitiza.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof Carolyne Nombo amesema NMB ni zaidi ya mdau kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu hasa kupitia ubunifu wake mkubwa pamoja na michango ya hali na mali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Prof Kitila Mkumbo, amesema uzinduzi wa huduma mpya uliyofanywa na NMB ni muhimu sana kwani fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi hazijawahi kutosha.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

error: Content is protected !!