TAASISI za umma nchini zimeshauriwa kushirikiana na taasisi binafsi katika jitihada za kuhakikisha teknolojia inatumika ipasavyo ili kupunguza ajali za magari nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Ushauri huo umetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa katika maadhimisho ya wiki ya Nenda kwa Usalama yaliyofanyika jijini Mwanza leo tarehe 14 Machi, 2023.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema taasisi za umma zina nafasi kubwa ya kushirikiana na taasisi za binafsi ambazo nyingi zimejikita katika teknolojia inayowezesha kuepusha ajali.
“Shirikisheni sekta binafsi ili kupata ujuzi na kujifunza kutoka kwao, hii itawawezesha kuboresha mifumo na hivyo kulinda maisha ya wananchi wetu ambayo yamekuwa yakipotea kwa ajali,” alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu aliongea hayo baada ya kupita katika banda la kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc na kujionea jinsi ambavyo mfumo wa kufuatilia magari ya kampuni na hivyo kuepusha ajali mahali pa kazi kwa miaka zaidi ya 10.

Aliongeza kwamba ili kudhibiti ajali zinazopoteza maisha ya wananchi, taasisi zina jukumu kubwa la kutafuta namna bora ya kulinda miundombinu na pia kuepusha majeruhi, “kwa miaka mitatu iliyopita (2020 – 2022) ajali nchini zilikatisha maisha ya watu 1582 na kusababisha majeruhi 4372, hili halikubaliki kabisa na tunatakiwa kulidhibiti.”
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Adam Malima amebainisha kuwa ni wajibu wa kisheria kwa kila mmiliki wa chombo cha moto kukatia bima chombo chake sio tu kwa sababu ili asikamatwe na askari wa usalama wa barabarani bali kwa faida yake, wamiliki wengine barabarani, abiria, na watembea kwa miguu.
“Kwa kuliona hilo, ningependa kuwapongeza Vodacom Tanzania Plc ambao ni mojawapo ya wadau wakubwa wa wiki hii ya usalama barabarani kwa miaka mingi mpaka imefikia wakati hatuendi kuwaomba tena udhamini, tunajua ni sehemu ya tukio hili. Wenyewe wanatumia teknolojia yao ya mawasiliano kuwa wabunifu kwa kuja bidhaa ambazo zinabadili hali ya Maisha ya Watanzania.

Kwa sasa wametuletea VODABIMA, baada ya kuona kuwa kuna changamoto kadhaa za kuzifikia huduma za bima, wao wakaamua kuitumia fursa ya mtandao mpana wa wateja walionao kuwarahisishia kuifikia huduma ya bima kwenye simu zao za mkononi. Ninaamini kila mmoja wenu hapa anamiliki simu ya mkononi, hivyo sioni sababu ya kutoanza kutumia huduma hii ambayo imekurahisishia kuendelea na shughuli zako kwa sababu itakuwezesha kukata bima popote pale ulipo bila kwenda ofisini,” alisema Malima.
Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama ambayo kitaifa inafanyika jijini Mwanza kuanzia Machi 14-17 ikiwa na kauli mbiu inayosema, ‘Tanzania Bila Ajali Inawezekana, Timiza Wajibu Wako’.
Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni alisema kuwa VODA BIMA inayopatikana kupitia huduma ya M-Pesa imekuja kufanya mapinduzi makubwa kwa kuondoa mlolongo kwa Watanzania ambao wanapatikana sehemu tofauti nchini kuzifikia huduma za bima kwa urahisi, kulipia kidogo kidogo kwa mwaka mzima, na kujulishwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno endapo inataka kuisha.

“Kupitia VODA BIMA inayopatikana kwenye M-Pesa anaweza akajiunga huduma ya bima kwa ajili ya chombo chake cha moto na kuanza kulipia kidogo kidogo kwa mwaka mzima. Pia, mteja atakuwa anajulishwa kwa kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno kujua mustakabali wa bima yake kama inakaribia kuisha ili alipie.
“Kwa sasa huduma hii inapatikana kwa wamiliki wa vyombo vyote vya moto kama vile magari madogo na makubwa, bajaji, na pikipiki. Lengo kuu la huduma hii ni kuisaidia serikali kuhamasisha wamiliki wote wa vyombo vya moto wanakuwa na bima kwa njia rahisi, salama, na haraka popote na muda wowote kwa kulipia kidogo kidogo,” alisema Mbeteni
Leave a comment