BENKI ya NMB imetenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyakazi wanaotaka kupata elimu ya juu au wale wanaohitaji fedha za kuwasomesha wategemezi wao. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Bidhaa hiyo mpya ya mikopo nafuu inayoleta ahueni kubwa katika ufadhili wa hasa elimu ya juu nchini imezinduliwa rasmi leo Jumanne jijini Dodoma na tayari inapatikana kwenye matawi yote ya benki hiyo yaliyotapakaa nchi nzima.

Mbali na vyuo vikuu, huduma ya ufadhili huu ambayo jina lake la kibiashara ni ‘NMB Elimu Loan’ itatolewa pia kwa ngazi zote za elimu zikiwemo shule za msingi na secondari hata vyuo vya ufundi.
Akitangaza kuanzishwa kwake rasmi leo tarehe 14 Machi 2023, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema mikopo inayotolewa kwa mwajiriwa yeyote inaanzia Sh 200,000 hadi Sh milioni 10 kwa mwaka kwa mtu mmoja.
Zaipuna amesema moja ya sifa za kupata mkopo huo, wenye riba ya asilimia tisa tu na ambao marejesho yake ni ndani ya miezi 12, ni kuwa mwajiriwa ambaye ni mteja wa NMB.
“Kuanzia leo (Jumanne), tumeanza rasmi kupokea maombi ya mkopo kwa ajili ya kugharamia elimu kwa wafanyakazi ambao mishahara yao inapita Benki ya NMB,” amesema Zaipuna.
“Huu ni utekelezaji wa makubaliano yetu na Wizara ya Elimu ya kuanza kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kupunguza utegemezi wa waajiriwa kwa bodi ya mikopo (HESLB) pale wanapotaka kujiendeleza kimasomo na pia kuwalipia ada vijana wao,” amefafanua.

Aidha, amesema NMB ina dhamira ya dhati katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha tasnia ya elimu na kuchangia kutoa elimu bora kwa wote huku ikiwa mstari wa mbele kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha za kuwafadhili wote wanaohitaji kujiendeleza kielimu.
“Tumezindua huduma hii hapa Dodoma leo lakini mikopo hii inatolewa katika matawi yetu yote nchi nzima,” afisa huyo amebainisha na kusema fedha zitakazotolewa zitaingizwa moja kwa moja katika akaunti ya shule au chuo husika na wala si vinginevyo.
“Ili kupata mkopo huu, fika tawi lolote la NMB na nakala ya mshahara wako, mtiriko wa ada, barua ya kujiunga na chuo na wafanyakazi wa Benki ya NMB watakupigia hesabu ya mkopo unaostahili kupata,” amesema Zaipuna.
Kwa kuanzisha huduma hii, NMB inakuwa imetimiza ahadi iliyoitoa mwaka jana yakuisaidia Serikali kuipunguzia HESLB mzigo wa kufadhili masomo ya juu na kuwa na vyanzo vipya vya mikopo ya elimu.
Mwishoni mwa mwaka 2022, benki hiyo ilifanya makubaliano na Serikali kupitia Wizara ya Elimu ya kuanza kuwakopesha wazazi kwa riba nafuu ili waweze kugharamia elimu yao ya juu au kuwasomesha wategemezi wao.
“Yote haya yanalenga kuendeleza juhudi za kukuza sekta ya elimu hapa nchini, na sisi kama wadau wakuu wa elimu, tumeona tutoe ushirikiano huu kwa serikali kwa manufaa ya watanzania wenzetu,” amesema Zaipuna huku akisisitiza kuwa NMB itaendelea kubuni suluhishi zaidi za kuboresha elimu na kuimarisha tasnia hiyo.

Katika hotuba yake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda aliyekuwa mgeni rasmi ameweka bayana matamanio yake ya kutaka kupatikana ufadhili zaidi ya kile ilichokifanya NMB kutoka kwa wadu wengine.
Aidha, amesema uwekezaji wa NMB ni kitu kikubwa kinachoongeza wigo wa watu kujisomesha na akaomba hela za mikopo hiyo zitumike kwa ajili ya madhumuni yaliyokosudiwa tu.
Waziri huyo amesema pamoja na bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kuongezeka kutoka Sh bilioni 464 Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani hadi Sh bilioni 657 kwenye mwaka huu wa fedha bado kuna uhitaji wa vyanzo vingine kama hiki kipya kilichoanzishwa na NMB.
“Nikiri kuwa nyie ni wadau wa kweli wa elimu nchini na mmeonyesha njia inayostahili kuzingatiwa na wadau wengine,” Prof Mkenda amesisitiza.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof Carolyne Nombo amesema NMB ni zaidi ya mdau kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu hasa kupitia ubunifu wake mkubwa pamoja na michango ya hali na mali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Prof Kitila Mkumbo, amesema uzinduzi wa huduma mpya uliyofanywa na NMB ni muhimu sana kwani fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi hazijawahi kutosha.
Leave a comment