Sunday , 5 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mahakama yakubali ombi la Serikali kuwahoji vigogo Chadema
Habari za Siasa

Mahakama yakubali ombi la Serikali kuwahoji vigogo Chadema

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, imekubali ombi la upande wa Serikali kuwahoji wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika kesi iliyofunguliwa na wabunge viti maalum 19. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uamuzi huo mdogo umetolewa tarehe 9 Machi 2023 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha, wakati akitoa uamuzi wa pingamizi lililowekwa na mawakili wa Chadema, dhidi ya ombi hilo lililowasilishwa na Wakili wa Serikali, Stanley Kalokola.

Jaji Mkeha aliuruhusu upande huo uhoji maswali ya dodoso yanayohusu hoja za kisheria.

Ni katika kesi Na. 36/2022 iliyofunguliwa na wabunge hao wakiongozwa na Halima Mdee, dhidi ya Chadema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupinga uamuzi wa chama hicho kuwafukuza kinyume Cha Sheria.

Akiwasilisha ombi hilo, Wakili Kalokola ameomba fursa hiyo akidai kwamba kwa mujibu wa sheria kama hawatapa nafasi hiyo, watakosa fursa ya kuwahoji wajumbe hao ambao ndio mashahidi katika kesi.


Wakili Kalokola alidai kuwa, wanaomba kuwafanyia dodoso wajumbe hao wa Chadema kwa kuwa katika kiapo chao kinzani aya ya nane wametengeneza ushahidi unaoathiri maslahi ya mjibu maombi wa pili na wa tatu (AG na NEC), na kwamba haki pekee waliyokuwa nayo pindi watakapoathirika ni kuwadodosa mashahidi hao.

“Sababu Sheria haielezi nini kifanyike pale wajibu maombi wawili wanapoathirika, ni wajibu wetu kumdodosa maana yake tusipofanya hivyo kila anachokisema ndiyo uhalisia, kwa minajili hiyo ni ombi letu wakati mashahidi walioapa kiapo kinzani pamoja wanadodoswa na waleta maombi basi mjibu maombi wapili na watatu wapewe fursa sawa kudodosa kwenye maeneo ambayo yamewaathiri,” amedai Wakili Kalokola.

Ombi hilo la Serikali linajiri baada ya mawakili wa wabunge viti maalum, kupewa nafasi ya kuwahoji maswali ya dodoso wajumbe sita wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, akiwemo Dk. Azavel Lwaitama, Ruth Mollel, Mary Joackim, Francis Mushi, Maulidah Anna Komu na Ahmed Rashid Hamis.

Vigogo hao wa Chadema, wameanza kuhojiwa leo mahakamani hapo, huku Dk. Lwaitama akifungua dimba hilo akifuatiwa na Mollel, ambapo wanahojiwa na mawakili wa kina Mdee wakiongozwa na Ipilinga Panya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mbatia ambwaga Selasini, mahakama yaamuru alipwe fidia

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemuamuru...

Habari za SiasaTangulizi

Mkulo afariki dunia, kuzikwa kesho Kilosa

Spread the loveALIYEKUWA Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kilosa (CCM), Mustafa...

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

error: Content is protected !!