MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari TPA imesema ujenzi wa miundombinu bora ya Bandari yenye mitambo ya kisasa na sahihi ya kuhudumia meli na shehena ni mojawapo ya vipaumbele vitano ambavyo viko kwenye Mpango Mkakati wake wa Nne wa mwaka 2021/22-2025/26) wa mamlaka hiyo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma (endelea).
Hayo yameelezwa leo tarehe 13 Agosti, 2022 na Mkurugenzi wa Mipango, ubora na Uthibiti vihatarishi Dk. Boniface Nobeji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mipango ya utekelezaji wa bajeti katika mwaka wa fedha 2022/23.
Aidha, amesema katika vipaumbele hivyo wanakusudia kuongeza shehena ya nchi jirani inayohudumiwa na bandari za Tanzania na kuimarisha masuala ya ulinzi, usalama na mazingira katika utoaji wa huduma pamoja na kuzingatia miongozo ya kimataifa iliyoridhiwa na nchi.
Ameeleza kuwa vipaumbele hivyo vinatekelezwa na TPA kupitia Mipango na bajeti za kila mwaka.
Kuhusu shehena ya magari iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 ilikuwa 203,932 sawa na ongezeko la asilimia 38 ya magari 147,566 yaliyohudumiwa mwaka uliopita (Julai 2020 hadi Juni 2021).
Dk. Nobeji ameeleza kuwa ili kuendelea kutekeleza vipaumbele ilivyojiwekea, katika mwaka wa Fedha 2022/2023, TPA imetenga bajeti yake kwa malengo mbalimbali.
Ameyatenga malengo hayo kuwa lengo la kwanza ni ukusanyaji wa mapato Jumla ya sh.bilioni 1,224.405.
Pia matumizi ni sh.bilioni 866.051 na ziada ya sh.bilioni 358.354 kabla ya kodi.
Aidha, ameeleza kuwa bajeti ya miradi ya uwekezaji ikiwemo vitendea kazi ni sh.bilioni 762.606 na sh.bilioni 662.493 ni mapato ya ndani huku sh. bilion 100.112 ikitoka Serikalini (Ruzuku kwa utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam).
Leave a comment