Tuesday , 7 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Mwili wa Balozi Kijazi wazikwa
Habari Mchanganyiko

Mwili wa Balozi Kijazi wazikwa

Spread the love

 

MWILI wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Tanzania, Balozi John Kijazi (64), umepumzishwa katika makazi yake ya milele. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tanga…(endelea).

Balozi Kijazi alifariki dunia tarehe 17 Februari 2021, kutokana na matatizo ya moyo, katika Hospitali ya Benjamini Mkapa, jijini Dodoma, alikokuwa anapatiwa matibabu tangu tarehe 1 Februari mwaka huu.

Maziko yake, yamefanyika, leo Jumamosi 20 Februari, 2021, kwenye Makaburi ya Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Augustino lililopo eneo la Manundu Korogwe, mkoani Tanga.

Mwili wa Balozi Kijazi uliingizwa kaburini majira ya saa 9:35 alasiri, kisha taratibu za viongozi wa Serikali, familia, ndugu jamaa na marafiki kuweka mchanga kaburini humo, zilianza.

Taratibu za mazishi ya mwili wa Balozi Kijazi zilifika tamati majira ya saa 10 jioni.

Kabla ya mwili huo kuzikwa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiambatana na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania, Venance Mabeyo, waliongoza shughuli ya kumuaga Marehemu Balozi Kijazi.

Mwili wa Balozi Kijazi, uliagwa kwenye misa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mt. Augustino, Korogwe, iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro, Askofu Telesphor Mkude.

Akizungumza katika ibada hiyo, Waziri Majaliwa amesema, Balozi Kijazi atakumbukwa kwa mengi katika Serikali ya Tanzania na nchi kwa ujumla kutokana na utendaji wake uliotukuka.

“Msiba huu ni mzito, kaka yetu ambaye yuko hapa mbele yetu ametangulia mbele ya haki, ametuachia mengi, tunalo jukumu kubwa kuyaenzi yale yote mema yaliyotamkwa na watu hapa ya kutenda mema kwenye utumishi wake na akiwa nyumbani. Jukumu la kumuenzi ni letu, ametuachia msingi imara tutekeleze hayo,” amesema Waziri Maajaliwa.

Enzi za uhai wake, Balozi Kijazi aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), nafasi aliyoitumikia kuanzia Agosti 2020 hadi umauti ulipomkuta.

Akitoa salamu za UDOM katika mazishi hayo, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Gaudensia Kabaka, amesema chuo hicho kimeumizwa na kifo cha Balozi Kijazi, na kwamba kitakumbuka unyekekevu wake na upendo.

“Pamoja na kazi zake za katibu mkuu kiongozi, aliweza kuwa na utumishi ndani ya chuo. Katika vikao vyote alivyokuja kitambulisho cha kwanza unyenyekevu wake na upendo wake. Na hali ya kutaka kufanya kazi na UDOM pamoja na kazi nyingi alizokuwa nazo serikalini,” amesema Kabaka.

Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Dk. Alfred Kimea amesema, wananchi wa jimbo lake wamepata pigo kufuatia kifo cha Balozi Kijazi, kwa kuwa enzi za uhai wake alikuwa msaada kwao.

“Sidhani kama nina maneno mazuri sana ya kumuaga baba yetu mpendwa, kimsingi mimi na wananchi wote wa Korogwe Mjini, tumeipokea kwa masikitiko makubwa habari ya kifo chake.”

“Alikuwa mlezi wetu, mshauri wetu wakati tulipohitaji ushauri. Alikuwa msaada mkubwa pale tulipohitaji msaada,” amesema Dk. Kimea.

Naye Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir amesema, marehemu Balozi Kijazi atakumbukwa kwa mema yake aliyoyafanya dunia, kupitia utendaji wake serikalini.

Balozi John Kijazi

Balozi Kijazi alipata shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1982. 1992 alipata shahada ya Uzamili kwenye Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham nchini Uingereza mwaka 1992.

1996 hadi 2002 alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kisha baadae alipandishwa cheo kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya wizara hiyo.

Balozi Kijazi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye wizara ya maendeleo ya miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006.

Kuanzia mwaka 2007-2016, aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania akihudumu katika nchi za India, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal, mwenye makazi yake jijini New Delhi India.

Ameacha mjane, Francisca Kijazi na watoto watatu wote wa kiume, David, Emmanuel na Richard.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

Habari Mchanganyiko

Mahakama yatoa uamuzi zuio dhidi ya Club House

Spread the loveMAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu jijini Dar es Salaam,...

Habari Mchanganyiko

GGML, OSHA yawanoa bodaboda 200 Arusha

Spread the loveZAIDI ya madereva bodaboda 200 wa jiji la Arusha wamepatiwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Serikali kuwakopesha wajasiriamali 18.5bn/- kupitia NMB

Spread the loveSerikali imetenga kiasi cha Sh 18.5 bilioni kwa ajili ya...

error: Content is protected !!