Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif aliwahi kupigwa mawe Zanzibar –Ismal Jussa
Habari za SiasaTangulizi

Maalim Seif aliwahi kupigwa mawe Zanzibar –Ismal Jussa

Spread the love

 

SAFARI ya Maalim Seif Sharif Hamad, katika harakati za kisiasa Visiwani, haikuwa rahisi. Ilipitia milima na mabonde; miamba na miba; dhuroba na kimbunga. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Maalim Seif ambaye amefariki dunia majuzi, jijini Dar es Salaam na kuzikwa kijijini kwake, Mtabwe, kisiwani Pemba, pamoja na kusindikizwa na maelfu ya watu katika safari yake hiyo ya mwisho, lakini mafanikio yake ya kisiasa, yalipitia misukosuko mingi.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Makamu huyo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, kabla ya kufikwa na umauti, tarehe 17 Februari 2021, aligombea urais wa Zanzibar katika chaguzi sita (1995, 2000, 2005, 2010, 2015, 2020), lakini hakuwahi kutangazwa kuwa mshindi.

Wafuasi wake wengi, waliamini Maalim Seif hajashindwa uchaguzi. Bali, amekuwa akiporwa ushindi wake.

Katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010, 2015, Maalim Seif aligombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), huku katika uchaguzi wake huu wa mwisho wa Oktoba mwaka jana, akigombea kupitia chama cha ACT-Wazalendo.

Ismail Jussa, akiweka udongo kwenye kaburi laMaalim Seif

Ismail Jussa Ladhu, mmoja wa watu waliofanya kazi kwa karibu na Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akiwa CUF na baadaye ACT- Wazalendo, anaeleza kiongozi huyo, alishawahi kupigwa mawe na wafuasi wake.

Jussa, anasimulia madhila aliyokutana nayo jabali hilo la kisiasa nchini, hususan katika harakati zake za kuhamasisha maridhiano Visiwani Zanzibar.

Akizungumza katika mjadala wa kumbukumbu ya hayati Maalim Seif, ulioendeshwa katika mtandao wa Youtube, jana tarehe 19 Februari 2021, Jussa amesema, mwanasiasa huyo aliwahi kupigwa mawe, kufuatia msimamo wake wa kufanya maridhiano na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Mwinyi, akimwapisha Maalim Seif

Alisema, Maalim Seif aliwahi kutukanwa na kurushiwa mawe katika mkutano wake wa hadhara alioufanya kwenye viwanja vya Demokrasia, Kibanda Maiti, mjini Unguja, baada ya kutoa msimamo wa kumtambua Amani Karume, kuwa rais wa Zanzibar.

Tukio hilo lililoacha historia kwa Maalim Seif, lilitokea mwaka 2005, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, na kisha Dk. Amani kutangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Jussa anaeleza, tukio hilo lilitokea baada ya wafuasi wa Maalim Seif kutokubaliana na msimamo wa mwanasiasa huyo, wa kuendelea kukubali kushindwa katika chaguzi hizo, na kisha kufanya mazungumzo na waliokuwa wapinzani wake.

“Yalipokuja maridhiano ya mwaka 2005, mnakumbuka tulipowenda hadharani mara ya mwanzo katika viwanja vya Demokrasia pale Kibandamaiti.

Maalim Seif wakati anazungumzia hoja ya kumtambua Rais Karume, ili kuweka hoja ya msingi ya maridhiano, watu walimzomea. Wakamtukana na hata kumrushia vitu juu ya jukwaa, lakini hakurudi nyuma,” amesimulia.

Jussa amesema, msimamo wa Maalim Seif kufanya maridhiano ya Serikali ya CCM kufuatia migogoro ya kiuchaguzi, ulimpa misukosuko mingi, na kwamba wakati mwingine alituhumiwa na baadhi ya watu kutumika katika kusafisha serikali iliyoko madarakani.

“Watu wengi hawajui masuala ya kuingia mazungumzo yaliyozaa miafaka na maridhiano hayakupata nafasi ndani ya vyama ambavyo amekuwemo.Alipokuwa CUF na hata ACT-Wazalendo,” ameeleza.

Jussa anasema, tuhuma za kuisafisha serikali iliyoko madarakani, Maalim Seif alizipata pia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, uliomuweka madarakani Dk. Salmin Amour.

Anasema, “katika uchaguzi wa mwaka 1995, baadhi ya watu hawakuona kama Dk. Amour ameshinda. Waliona kama vile jitihada za kuisafisha serikali na kuhalisha ushindi usiokuwa wake. Lakini tofauti na sote, Maalim Seif aliona fursa, sababu alikuwa anaamini tumepata pakuanzia.”

Dk. HUssein Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa mmoja wa vijana walioanzisha vuguvugu la mageuzi Zanzibar na kupewa jina la – Kamahuru – amemtaja Maalim Seif kama mtu mvumilivu na asiyeyumbishwa.

Anasema, hata CCM ilipokwenda kinyume na maazimio ya maridhiano yaliyoafikiwa katika nyakati tofauti, alikubali kurudi mezani tena kufanya majadiliano.

Anasema, “licha ya kupingwa na baadhi ya viongozi wa chama na hata wafuasi wake, Maalim Seif alithamini maisha ya Wazanzibari, ndiyo maana hakutaka kutumia njia za maandamano kudai haki, hasa inapotokea migogoro ya kiuchaguzi, badala yake alipenda kutumia njia za maridhiano.”

Kwa mujibu wa Jussa, hata maridhiano yaliyofanyika hivi karibuni kati ya Maalim Seif na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020, yalipingwa na baadhi ya watu ndani na nje ya ACT-Wazalendo.

“Hili la mwisho, sisi wengine tulikuwa juu ya vitanda tunauguza majeraha, alipochukua hoja ya kuleta maridhiano watu walimlaumu mno. Lakini hatimaye nadhani ushahidi umeonekana, hata waliompinga waliona Maalim Seif aliona mbali. Siku zote alisimamia anachoamini, hata dunia nzima ikimpinga,” ameeleza Jussa.

Wakati wa uhai wake, Maalim Seif alikiongoza chama chake za awali – The Civic United Front – Chama cha Wananchi (CUF), kufanya maridhiano na serikali ya CCM mara tatu.

Maalim Seif Sharrif Hamad, wakati alipokuwa Mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo

Baada ya kwanza ilikuwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Hatimaye maridhiano ya 2010 yalifanikisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), baada ya Katiba ya Zanzibar kufanyiwa marekebisho na kuwekwa kifungu kinachoruhusu Makamu wawili wa Rais.

Makamu wa kwanza akitoka chama cha upinzani kilichoshika nafasi ya pili kwa idadi ya kura za urais, huku makamu wa pili akitoka chama kilichoshinda kiti cha urais.

Kufuatia marekebisho hayo ya Katiba, Maalim Seif alishiriki kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), mara mbili kwa kukubali kuwa Makamu wa Kwaza wa Rais, moja akiwa CUF mwaka 2010 hadi 2015 na nyingine akiwa ACT- Wazalendo mwaka 2021.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Maalim Seif aligoma kuingia kwenye serikali, kufuatia hatua ya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuamua kufuta uchaguzi huo na matokeo yake, kinyume na taratibu.

 

Jecha alidai kuwa aliamua kufuta uchaguzi huo, baada ya kubaini kuwapo kwa hitilafu kwenye zoezi la upigaji kura na uhesabu wa matokeo, jambo ambalo lilipingwa na waangalizi wote wa kimataifa.

Wakati Jecha anatangaza kufuta uchaguzi, Maalim Seif alikuwa ameshakusanya matokeo katika vituo vyote na kufanya majumuisho yaliyomhakikishia ushindi.

Kama hiyo haitoshi, wakati Jecha anafuta uchaguzi na matokeo yake, uchaguzi wa rais wa Muungano na wabunge wa Bunge hilo, ambao ulisimamiwa na watu walewale, ulikuwa unaendelea kama kawaida; na matokeo ya wajumbe wa Baraza la Wawawakilishi, yakiwa tayari yametoka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!