Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Vigogo wazidi kukatika, Dk. Likwelile awafuata
Habari za SiasaTangulizi

Vigogo wazidi kukatika, Dk. Likwelile awafuata

Spread the love

 

ALIYEKUWA katibu mkuu wa wizara ya Fedha na Mipango, katika serikali ya Tanzania, Dk. Servasius Beda Likwelile, amefariki dunia. Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Taarifa za kifo chake, zimetolewa na mke wake, Vick Kamata Likwalile, ambaye amesema, mume wake huyo, amekutwa na mauti, usiku wa kuamikia leo, Jumamosi, tarehe 20 Februari 2021, katika hospitali ya Regency, jijini Dar es Salaam.

Kifo cha Dk. Likwalile, kinakuja siku tatu, baada ya taifa kuwapoteza viongozi wawili mashuhuri, Makamu wa Kwanza wa Rais Visiwani, Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.

Naye Padre wa Parokia ya Kristo Mfalme, Kibaoni, mkoani Singida, Parick Njiku, amefariki dunia, kwenye hospitali ya Benjamini Mkapa, mjini Dodoma.

Taarifa ya kifo chake, zimetolewa na Mhashamu Baba Askofu, Edward Mapunda, ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Singida.

Katika taarifa yake, Askofu Mapunda amesema, “Padre Patrick Njiku, aliyekuwa anafanya Utume wake katika Paroka ya Kristo Mfalme Kibaoni, amekutwa na mauti jana, tarehe 19 Februari, mkoni Dodoma.”

Baba Mhashamu Askofu Mapunda amesema, misa ya kuuaga mwili wa marehemu Padre Njiku, itafanyika tarehe 23 Februari, katika Parokia ya Kristo Mfalme Kibaoni, alipokuwa anafanyia kazi zake za utume.

Askofu Mapunda amesema, mazishi ya Padre Njiku, yatafanyika Jumanne, tarehe 23 Februari 2021, saa 4:00 asubuhi.

Yatatanguliwa na Misa Takatifu katika Parokia ya Mt. Leo Nkuu Makiungu, mkoani humo.

Maalim Seif

Kupatikana kwa taarifa za vifo vya Padre Njiku na Dk. Likwelile, kumekuja katika kipindi ambacho watu kadhaa mashuhuri nchini Tanzania, wakiwamo viongozi wa madhehebu ya kidini na wanasiasa, wameripotiwa kufariki dunia, nchini Tanzania.

Mbali na vifo vya Maalim Seif (77) na Balozi Kijazi (64), wengine walioripotiwa kufariki dunia hivi karibuni, ni pamoja na Paroko wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mwananyamala, Benedict Ndeyekiyo na Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Paroki ya Chang’ombe, Ernest Boyo.

Wengine, ni Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la taifa, Charles Mngeleza; aliyekuwa waziri mwandamizi katika Serikali ya Ali Hassani Mwinyi na Benjamin Mkapa, Arcado Ntagazwa; na Agen Mwandosya, baba mdogo wa waziri wa zamani katika serikali ya Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, Prof. Mark Mwandosya.

Katika orodha hiyo, wapo pia mawaziri wa zamani, Bakari Harithi Mwapachu na Mohammed Seif Khatibu; mbunge wa Muhambwe, Atashasta Nditiye; mawakili 25 wanachama wa chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania, (Tanroad, mkoa wa Dar es Salaam, Ngusa Julius Ndema na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (Ruco), mkoani Iringa, Profesa Gaudence Mpangala.

Dk. likwelile

Wengine waliokutwa na mauti ghafla, ni mfanyabiashara mashuhuri jijini Dar es Salaam, George Lwakatare; Balozi Eva Nzaro, mtoto wa aliyekuwa Jaji Goodwill Korosso, aliyefahamika kwa jina la David Korosso na mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha ITV na Radio One, Vedasto Msungu (59).

Mbali na hao, vyanzo mbalimbali vya taarifa, ikiwamo mitandao ya kijamii, vinaonyesha kuwa makumi ya raia wanaripotiwa kufariki dunia kila siku, katika wakati huu, ambapo dunia imegubikwa na wimbi kubwa la maambukizi ya virusi vya Covid 19.

Hata hivyo, serikali kupitia kwa waziri wake wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dorothy Gwajima, imekuwa ikieleza kuwa Tanzania haina maambukizi ya Covid19, bali ametaka wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kutumia dawa za asili.

John Kijazi

Amesema, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari kutokana na kuenea kwa ugonjwa huo katika mataifa jirani.

Ameongeza, “…kwa hivyo, ninachotaka kusema hapa ni kwamba, nchi yetu ipo salama. Tunasikia kwa jirani huko kuna shida, usisubiri vitoke kwa jirani vije kwasababu tunaingiliana maisha, sisi tunajiandaa kwa maisha.”

Gwajima amepiga marufuku matangazo ya wagonjwa wa corona wala vifo vinavyodaiwa kutokana na ugonjwa huo, kutolewa hadharani na mamlaka zisizohusika.

Kabla ya kukutwa na mauti, Dk. Likwalile, alikuwa mhadhiri mwandamizi katika chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alirejea katika chuo hicho kuendelea na kazi yake ya kufundisha, takribani miaka minne iliyopita, muda mfupi baada ya kuondolewa Hazina.

Katika kipindi cha uhai wake na hasa alipokuwa katibu mkuu wa Hazina, Dk. Likwalile, alisaidia sana kujenga uchumi wa taifa, ikiwamo kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na nchi wahisani, kama vile, shirika la fedha la kimataifa (IMF) na Banki ya Dunia (WB).

Vedasto Msungu

Alikuwa mmoja wa wachumi walioamini katika matumizi mazuri ya fedha za mikopo na misaada ambayo serikali ya Tanzania, ilikuwa inapata kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa IMF na WB, huko Washington DC, Marekani, Oktoba mwaka 2014, Dk. Likwalile alisema, ni muhimu mashirika hayo yakabadilisha mtazamo wake kwa nchi za Afrika, hasa kwenye utoaji wa mikopo.

Alisema, “shida siyo kukopa. Ni matumizi ya hiyo mikopo. Katika nchi nyingi, mikopo inayochukuliwa, haitumiki kwa malengo yanayotakiwa, hivyo ni muhimu kwa mashirika hayo, kufuatilia kufuatilia matumizi yake.”

Mkutano kati ya mashirika hayo, ulikutanisha magavana wa bodi za taasisi hizo mbili na wawakilishi kutoka nchi wanachama. Dk. Likwalile wakati huo, alikuwa katibu mkuu Hazina.

Atashasta Nditiye

Aidha, Dk. Likwalile alisaidia sana serikali kurejesha heshima yake kwa wahisani, ikiwamo Marekani, ambapo tarehe 1 Agosti 2016, serikali ilijifunga kwenye mkataba wa miaka mitano na shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).

Katika mkataba huo, Dk. Likwelile, alisaini kwa niaba ya Jamhuri, mkataba wa miaka mitano uliolenga kusaidia serikali kufikia mageuzi yake ya kiuchumi, ili kuweza kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wa USAID, mkataba huo ulisainiwa na mkurugenzi wake mkazi, Sharon Cromer.

Charles Mngeleza

Chini ya mkataba huo, mwaka huo huo 2016, Marekani kupitia shirika lake hilo, ilitarajia kuwekeza nchini dola za Kimarekani 407 milioni katika sekta mbalimbali, ikiwamo afya, kilimo, usimamizi wa maliasili, nishati na utawala wa kidemokrasia.

Dk. Likwalile alifunga ndoa na Vick Kamata, aliyekuwa mbunge wa Bunge la Muungano (20015 hadi 2020), kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya mkewe wa awali kufariki dunia, Mei 2014.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Bunge labaini madudu mfumo ukusanyaji mapato, h’shauri tatu kikaangoni

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali...

Habari za Siasa

Mkuu wa wilaya ya Rungwe azindua vyumba sita vya madarasa vya thamani ya 64 mil

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amezindua vyumba...

Habari za Siasa

Mbunge afurahia mabilioni ya Samia kutua jimboni

Spread the love  MBUNGE wa Igunga, Nicholas Ngassa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji...

Habari za Siasa

PIC yaishauri Serikali kuanzisha mfuko wa uwekezaji kusaidia mashirika ya umma

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji...

error: Content is protected !!