Sunday , 5 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mgombea urais NCCR-Mageuzi kugawa bure taulo za kike shuleni
Habari za Siasa

Mgombea urais NCCR-Mageuzi kugawa bure taulo za kike shuleni

Spread the love

YEREMIA Kulwa Maganja, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, ameahidi kugawa taulo za kike ‘Pad’ bure katika shule zote, atakapofanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020.Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Maganja ametoa ahadi hiyo wakati akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha East Afrika (EATV), kuhusu masuala yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya NCCR-Mageuzi.

Maganja ametoa ahadi hiyo alipoulizwa kuhusu changamoto ya watoto wa kike waliobarehe kukosa taulo za kujihifadhi wakati wa siku zao za hedhi.

Sambamba na hilo, Maganja ameahidi kutenga maeneo maalumu katika kila shule yatakayotumiwa na watoto wa kike kujihifadhi wakati wa hedhi.

“Na katika miundombinu yetu ya shule, lazima kuwe na nafasi ya wasichana hawa kujistili wanapokwenda katika vipindi hivyo ambavyo vitawafanya watake taulo na zitafika katika shule kama chaki zinavyofika kufundishia darasani ,” amesema Maganja.

Yeremia Maganja wa NCCR-Mageuzi kuwa mgombea urais wa Tanzania

Maganja ameahidi kuweka mama mlezi wa wasichana katika shule zote atakayesimamia malezi ya wanafunzi hao.

“Kwanza kabisa, shule hizi zote tutaweka utaratibu ambao upo ili kuifanya shule iende vizuri kwa malezi ya watoto wa jinsia tofauti, inatakiwa kuwe na mama mlezi wa wasichana ambaye anajua malezi ya wasichana,” ameahidi Maganja.

Aidha, Maganja ameahidi kuleta mageuzi katika sekta ya elimu, pindi atakapochaguliwa na Watanzania kuwa rais wao.

Katika uboreshaji wa sekta hiyo, Maganja ameahidi kubadili mfumo wa utoaji elimu, ili Taifa liwe na mfumo wa elimu inayotoa mafunzo ya elimu kazi kwa wahitimu kwa lengo la kukidhi matakwa ya soko la ajira.

“Mapato ya Serikali yatatumika kwenda katika elimu, kuja na elimu nzuri itakayofundisha elimu kazi, maana yake mitaala yetu tuibadilishe ili watu wawe na elimu kazi, yaani ametoka ana ujuzi na maarifa ya kwenda kuzalisha aidha ameajiriwa au amejiari, au kuweza kushindana katika soko la ajira,” amesema Maganja.

Maganja amesema ataanza kuboresha miundombinu ya shule na vyuo vyote ili ziwe na mazingira mazuri ya ufundishaji.

“Cha kwanza sisi tunaamini kwamba ili uweze kutoa elimu inayotoa elimu chanya kwa maendeleo ya taifa lolote lazima miundombinu ya kutolea elimu iwe bora. Suala la upungufu wa vyoo shuleni au suala fulani hayo katika Serikali yetu hayatakuwepo tena ili kusiwe na vikwazo kwa shule kutoa elimu bora,” amesema Maganja.

Suala la pili aliloahidi Maganja kufanya ili kuboresha sekta ya elimu ni kutoa mafunzo kwa watu wanaohusika na sekta ya elimu hasa walimu.

Tatu, ni kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kulipa stahiki zao na kununua vitendea kazi.

“Lazima wanaotoa elimu hiyo yani walimu lazima wawe na mafunzo stahiki kila hatua ya elimu. Lazima kuwe na rasilimali fedha ya kuwafanya walimu hao wapate stahiki zao bila shida na vitendea kazi bila matatizo.”

“Matokeo yake yatazalisha wahitimu wakiwa na uweledi wa kutosha kwa kila ngazi,” amesema Maganja.

Wakati huo huo, Maganja amesema, akifanikiwa kuwa Rais wa Tanzania Serikali yake haitabagua katika suala la utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

“Mimi Maganja ambaye nakuja kwa Watanzania kuomba ridhaa ya kuongoza, sitaongoza taifa la kiubaguzi, nitahakikisha fursa tunazipata sawa, kwa hiyo suala la mikopo halitakuwepo kwa vyuo vikuu na halitakuwepo kwenye vyuo vya ufundi,” amesema Maganja.

Maganja amesema “Ni lazima kuwe na mtizamo mpya wa kujenga taifa hili, kujenga taifa linalokwenda kuzalisha ni lazima watu wapewe elimu stahiki kwa wingi ili waweze kujenga taifa.”

“Hilo ndilo jambo tutakalofanya, ni haki mtoto kupata elimu na itakuwepo Kikatiba kusema huyu apewe mkopo huyu asipewe ni ubaguzi.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mbatia ambwaga Selasini, mahakama yaamuru alipwe fidia

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemuamuru...

Habari za SiasaTangulizi

Mkulo afariki dunia, kuzikwa kesho Kilosa

Spread the loveALIYEKUWA Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kilosa (CCM), Mustafa...

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

error: Content is protected !!