Tuesday , 7 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Uchaguzi mkuu 2020: ZEC yavipa jukumu vyama vya siasa
Habari za Siasa

Uchaguzi mkuu 2020: ZEC yavipa jukumu vyama vya siasa

Spread the love

MKURUGENZI wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarus Faina amevitaka vyama vya siasa kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum katika uchaguzi kwani hilo si jukumu la tume hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Pia, amezitaka asasi za kiraia kuhamasisha mambo mawili ili wanawake washiriki katika siasa, kwanza, kuwaondolea woga na pili kuwawezesha kifedha ili wakagombee katika majimbo. 

Faina ameyasema hayo leo Alhamisi tarehe 2 Julai 2020 wakati alipokutana na Jukwaa la Katiba Tanzania, (JUKATA) chini ya mwamvuli wa Ushiriki Tanzania kuzungumzia masuala mbalimbali ya uchaguzi.

Faina amesema, ZEC haina uwezo wa kutengeneza mazingira ya ushiriki wa makundi maalum ndani ya vyama  vya siasa bali vyama hivyo viwajibike kwa kuwateua wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika nafasi mbalimbali.

“Katika uchaguzi mkuu ujao, tunataka muwasaidie wanawake, kwanza waondoe woga na pia, kuwe na mfuko maalum ambao utawasaidia  kupata fedha za kufanya kampeni, wengi wao hawana uwezo wa kiuchumi,” amesema.

      Soma zaidi:-

Amesema, bila kufanya hayo, asilimia ya ushiriki wa wanawake katika ubunge, baraza la wawakilishi na udiwani, itabaki ile ile asilimia 40.

Mkurugenzi huyo amesema, vyama vya siasa ndivyo vimekuwa na udhaifu wa kuchagua wanawake kushika nafasi ndani ya vyama au nje  na akatolea mfano wawakilishi katika kamati za tume ya uchaguzi visiwani humo.

“Tuna vyama 19 lakini katika kamati za tume zilizo chini ya ZEC, kuna  wanawake watatu tu, ambao pia wametoka katika vyama vidogo na si vyama vikubwa vyenye majina, licha ya kuwaambia wateue wanawake katika nafasi hizo” amesema.

Amesema, bado kuna safari ndefu ya kuleta usawa wa makundi maalum lakini jitihada hazina budi kuanzia ndani ya vyama vya siasa hadi hapo sheria ya mgombea binafsi itakapopitishwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mshauri wa JUKATA, Deus Kibamba amesema, jukwaa hilo chini ya uratibu wa Ushiriki Tanzania, walikwenda kushauriana na ZEC juu ya namna bora ya kuwezesha ushiriki wa makundi maalum.

“Ingawa kuna ibara za katiba na vifungu vya sheria pamoja na kanuni, ambavyo vinazuia ubaguzi wa makundi maalum, utekelezaji wake umekuwa ni hafifu na hivyo ZEC ina uwezo wa kushadidia ushiriki wa makundi hayo katika uchaguzi mkuu ujao,” amesema

Kibamba amesema, ni vyema kwa ZEC, kuboresha mfumo wake wa unasaji taarifa ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu zinazobainisha ushiriki wa makundi hayo maalum.

Katika hilo, Faina amesema, itatoa taarifa za walioajiandikisha kupiga kura visiwani humo itakayoonyesha idadi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutokana na fomu iliyoandaliwa ikiwa  na vielelezo.

Kaimu Mwenyekiti wa Ushiriki Tanzania, upande wa Visiwani, Salma Saadat alisema ingawa wanawake ni wachache katika kamati hizo zilizo chini ya ZEC lakini angalau wapo wawakilishi wanawake.

“Lakini kwa mwaka huu sisi asasi tunataka kuwe na siasa za kistaarabu zisizo na matusi. Lakini zaidi hasa ZEC iandae vifaa  kwa watu wenye ulemavu wakati huu wa uchaguzi,” alisema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Jacob, Malisa wapandishwa kizimbani kwa mashtaka ya uongo mitandaoni

Spread the loveMKURUGENZI wa Shirika la Haki, Godlisten Malisa na mwanachama wa...

BiasharaHabari za Siasa

Bunge laitaka Serikali kudhibiti ufisadi miradi ya mkakati

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka Serikali kuimarisha...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Wizara ya Uchukuzi yaomba kuongezewa bajeti na Bunge

Spread the loveWIZARA ya Uchukuzi imeliomba Bunge liidhinishe bajeti yake kwa mwaka...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali kutafuta mwekezaji mwingine Bandari ya Dar es Salaam

Spread the loveSERIKALI inaendelea kutafuta mwekezaji mwingine atakayeendesha gati namba nane hadi...

error: Content is protected !!