SERIKALI imeeleza kuwa, kwa sasa hakuna kesi yoyote iliyofunguliwa na kampuni ya Madini ya Acacia Mining PLC katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi ya London (LCIA). Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, leo tarehe 9 Novemba 2018 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuna mashauri mawili namba UN 173686 na 1736867 yaliyofunguliwa LCIA na kampuni za madini za Pangea na Bulyanhulu.
“Kwa sasa hakuna kesi yoyote katika mahakama za usuluhishi London iliyofunguliwa dhidi ya serikali na kampuni ya Acacia Mining. Shauri Na. LCIA Arbitration UN 173686 lililotajwa na shauri UN 1736867 yamefunguliwa mnamo Julai 3, 2017 na makampuni mawili ya madini ya hapa Tanzania ya Pangea Minerals ltd na Bulyanhulu Gold Mining Ltd,” amesema.
Prof. Kbaudi ameeleza kuwa,utetezi wa serikali kwenye kesi hizo umekwisha wasilishwa LCIA, ambapo makampuni hayo yanaendelea na mashauri hayo kwa madai ya kulinda masilahi ya wanahisa wao.
“Napenda kulijulisha bunge lako tukufu kwamba kwa mujibu wa masharti katika mikataba ya kimataifa, kanuni na desturi zinazosimamia mashauri ya usuluhishi kimataifa, inaelekeza masuala ya kesi yaliyopo kwenye vyombo vya usuluhishi ni siri mpaka pale mahakama au baraza husika la usuluhishi itakapotaka kuyaweka wazi,” amesisitiza Prof. Kabudi.
Katika swali lake, Zitto alihoji kuwa, kwa nini serikali ishtakiwe na kampuni hizo wakati ilikwisha fanya mazungumzo na kampuni mama ya Barrick ambayo ni mmiliki wa Acacia inayosimamia kampuni za madini za Pangea na Bulyanhulu, na serikali kuahidiwa kishika uchumba kiasi cha dola 300 Milioni (Sh. 700 Bilioni).
Leave a comment