Tuesday , 7 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Madiwani wanne wa CUF watimuliwa Tanga
Habari za SiasaTangulizi

Madiwani wanne wa CUF watimuliwa Tanga

Spread the love

KUFUKUZWA KWA MADIWANI WETU WANNE WA TANGA!

Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, jana jioni (09 Julai 2018) ametangaza kuwafukuza udiwani, madiwani wanne wa The Civic United Front (CUF), kati yao wawili wakiwa ni madiwani wa kuchaguliwa kwenye kata (akiwemo diwani ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Tanga Mjini wa chama chetu), madiwani wawili ni wa Viti Maalum.

Mkurugenzi huyo amechukua uamuzi huo baada ya kupokea barua ya Magdalena Sakaya, ambaye CCM na Dola wanamtumia ipasavyo (kupitia kwa Lipumba) ili kuhakikisha hadi mwaka 2020 maeneo ambayo CUF ina nguvu sana, madiwani na wabunge wawe wamesambaratishwa ili kuirahisishia kazi CCM.

Kwa sababu jambo hili limetokea ghafla, na likifanywa na vibaraka ambao CCM na Dola inalazimisha kuwakaimisha uongozi wa chama, mawakili wameanza hatua za kisheria ili kupambana dhidi ya jambo hilo.

Taarifa tulizonazo zinaonesha kwamba, tayari CCM na Dola vimeshaielekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza kata hizo kuwa wazi ndani ya wiki ijayo ili uchaguzi ufanyike haraka na madiwani wapya wa CCM washinde. Pia, Lipumba ametakiwa kupeleka madiwani wa viti maalum wawili haraka sana na kuhakikisha kuwa madiwani hao wanakuwa wale wanaoiunga mkono CCM.

Tanga ni jiji ambalo CUF ilishinda umeya mwaka 2015 kwa kupata madiwani wengi, kwa makusudi dola na CCM wakajitangazia kuchukua umeya ilihali aliyeshinda kwa kura za baraza la madiwani, ni diwani wa CUF (ambaye ni miongoni mwa waliotangazwa kufukuzwa jana na Mkurugenzi kwa amri ya Sakaya na Lipumba).

Mkakati wa sasa ni kama ule uliotumiwa bungeni (kesi ziko Mahakama Kuu) ambapo wabunge halali wa viti maalum wa CUF walifukuzwa uanachama na Lipumba na Sakaya na kisha kwa kasi kubwa Lipumba akateua wabunge wake binafsi wapatao nane ambao wamo bungeni hivi sasa na wote majuzi wakiiunga mkono kwa mbwembwe bajeti hewa iliyowasilishwa na serikali ya CCM (hawa ni wale wabunge ambao kila wakisimama bungeni CCM nzima inashangilia).

Nawaomba wanachama na madiwani wa CUF Tanga, ambao asilimia 99 wamekuwa na msimamo wa kukilinda chama dhidi ya wasaliti wa ndani, waendelee kuwa imara na watulivu wakati masuala haya yakishughulikiwa kwa njia za kutafuta haki ambazo zimo ndani ya uwezo wetu.

Mapambano ya ndani ya chama chetu, ya kukilinda na kukiokoa chama, yasingelichukua hata siku moja kama yasingelikuwa yanasimamiwa na na kufadhiliwa na CCM, Usalama Wa Taifa, Vyombo Dola, Serikali, Msajili wa Vyama vya Siasa n.k. tena vyombo hivyo vikifanya hivyo usiku na mchana kwa kumtumia Lipumba na genge lake.

Mapambano haya si rahisi kwa sababu tunapambaba na dola nzima na rasilimali zake zote. Nawaomba tuendelee kusimama imara mpaka haki itakapotamalaki. Haki huweza kucheleweshwa tu, haipokonyeki.

Mtatiro J,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
The Civic United Front (CUF),
10 Julai 2018.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Jacob, Malisa wapandishwa kizimbani kwa mashtaka ya uongo mitandaoni

Spread the loveMKURUGENZI wa Shirika la Haki, Godlisten Malisa na mwanachama wa...

BiasharaHabari za Siasa

Bunge laitaka Serikali kudhibiti ufisadi miradi ya mkakati

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka Serikali kuimarisha...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Wizara ya Uchukuzi yaomba kuongezewa bajeti na Bunge

Spread the loveWIZARA ya Uchukuzi imeliomba Bunge liidhinishe bajeti yake kwa mwaka...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali kutafuta mwekezaji mwingine Bandari ya Dar es Salaam

Spread the loveSERIKALI inaendelea kutafuta mwekezaji mwingine atakayeendesha gati namba nane hadi...

error: Content is protected !!