February 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Watoto wenye ulemavu waomba Bima ya Afya bure

Spread the love

WAZAZI na walezi wenye watoto walemavu wa akili na viungo nchini wameiomba Serikali kuwakatia Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu ya watoto wao kufuatia kukabiliwa na changamoto za kiuchumi kutokana na kutumia muda mwingi kuwahudumia watoto hivyo kupunguza muda wa kufanya shughuli za kujiongezea kipato. Anaripoti Christina Haule … (endelea).

Wakizungumza wakati wa uhamasishwaji wazazi wenye watoto walemavu wa akili na viungo kutoka maeneo ya Gairo Kusini, Kilosa Kusini na Mvomero Kusini uliolenga kuelimishana namna ya malezi wazazi hao walisema kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambaapo nyingi ya hizo zin atokana na uchumi mdogo walionao.

Mmoja wa wazazi wa watoto wenye ulemavu wa akili na viungo, Khadija Mniso mkazi wa Kilosa, amesema kuwa wanatumia muda mwingi kuwahudumia watoto hao kufuatia watoto hao mara nyingi kutokuwa na uwezo wa kusema kama wanataka kujisaidia haja kubwa ama ndogo na hivyo kuchafua nguo muda wote.

Naye Asha David Mzazi wa mtoto mwenye ulemavu amesema kuwa watoto wao wamekuwa wakinyanyapaliwa mitaani, kutengwa kwenye mikusanyiko ya watu na hivyo mara nyingi kubaki mikononi mwa wazazi au walezi wao.

Amesema kuwa kufuatia kunyanyapaliwa na kutengwa wazazi wamekuwa wakitumia muda mwingi wakiwa na wao hivyo ni vema Serikali ikawakatia Bima ya Afya ili waweze kupata matibabu.

Kwa upande wake, Ofisa Tarafa ya Mvomero, Winfred Kipako amesisitiza wazazi kuacha kuwapeleka watoto kwa waganga wa jadi pindi wanapougua kwani ulemavu mwingine unasababishwa na tiba zisizo salama.

Awali Mkurugenzi wa Shirika la Eric Memorial Foundation (EMFERD), Josephine Bakhita amesema kuwa wameamua kuwakutanisha wazazi na watoto wenye ulemavu ili kujadili changamoto zinazo wakabili na kubadilishana uzoefu.

error: Content is protected !!