Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Kaya 28 zakosa makazi kutokana na mvua
Habari Mchanganyiko

Kaya 28 zakosa makazi kutokana na mvua

Spread the love

ZAIDI ya Familia 28 zilizopo katika kijiji cha Milengwelengwe Kata ya Mngazi Tarafa ya Bwakira chini wilayani Morogoro hazina mahali pa kuishi baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na kuezua na kuangusha nyumba walizokuwa wakiishi, anaandika Christina Haule.

Diwani wa Kata ya Bwakira chini Pesa Mohamed Pesa amesema kuwa mvua hiyo ilinyesha mwishoni mwa wiki, saa 11 jioni ndani ya masaa mawili huku ikiambatana na upepo mkali na kusababisha  nyumba hizo zaidi ya 28 kuezuliwa paa huku zingine zikidondoka chini na kusababisha majeruhi waliokimbizwa katika hospitali ya Mngazi kwa matibabu.

Pesa amesema kuwa wananchi waliojeruhiwa waliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kuonekana hali zao sio mbaya sana huku akina mama na watoto wakiteseka zaidi kwa kukosa mahali pa kuishi huku wakisaidiwa na majirani kwa kuwapa hifadhi ya muda.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho, Salum Ngotwike amesema baadhi ya watu wamejeruhiwa vibaya na mabati hivyo hawawezi kujihudumia wala kukarabati nyumba zao kutokana na maumivu waliyonayo na kuomba viongozi husika kuwasaidia wakazi hao.

Aidha amesema kuwa baadhi ya nyumba zimebomoka upande na hivyo kufanya watu kuishi upande mwingine wa nyumba jambo ambalo ni hatari huku wengine wakiwa wamehifadhiwa na majirani na ndugu ingawa hawapati huduma zote muhimu kama chakula.

“Mvua ilikuwa nyingi kiasi ila upepo ulikuwa mkali sana na kusababisha paa za nyumba kuezuliwa, nimepiga simu ngazi ya kata ili na wao walipeleke mbele swala hili ili watu hawa wapatiwe msaada wa haraka hasa akina mama na watoto,” amesema Ngotwike.

Kwa upande wao waathirika wa mvua hiyo, Salehe Hussen na Hadija Makombora wamesema kuwa wamepata hasara kubwa kwa kubomokewa na nyumba zao huku baadhi ya vitu kama vitanda, vyombo na chakula walichokuwa wamekihifadhi kuwa vimeharibika na kuwaacha hawajui la kufanya.

“Tunaomba Serikali itusaidie, tunateseka sana, mimi mwanangu kaangukiwa na tofali mguu umevimba hawezi hata kutembea, sina pa kuishi na wanangu kwani mimi ni mjane nani atanisaidia zaidi ya serikali?” amesema Hadija.

Mvua hizo zilizoanza kunyesha mwishoni mwa mwezi wa pili mkoani hapa zinanyesha kubwa katika baadhi ya maeneo na kusababisha hasara huku maeneo mengine ikinyesha kwa wastani sana.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

error: Content is protected !!