MKUU wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo amesema mwananchi yeyote atakayeshindwa kutoa ushirikiano wa kujua idadi ya mifugo aliyo nayo atatiwa nguvuni, anaandika Mwandishi Wetu.
Akizungumza wakati wa kuzindua kazi ya ukusanya takwimu iliyofanyika kwenye kata ya Olbalbald, alisema serikali imeamua kufanya sensa ili kujua idadi sahihi itakayoweza kuwasaidia wananchi wa eneo hilo kupata misaada.
“Kujua idadi ya mifugo itatusaidia serikali kujua hata kama tunaleta chanjo za mifugo basi tujue ni idadi gani na pia kujua mifugo iliyo ni ya eneo hilo au la,” alisema.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji, Edward Maura, alisema kupitia ukusanyaji wa takwimu ya idadi ya watu na mifugo kwenye eneo hilo, litaweza kusaidia kutoa dira ya maendeleo hasa katika kubainisha maeneo pamoja na matumizi yake.
Amesema eneo hilo linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo uhaba wa maji, barabara na huduma za kijamii kwa hiyo amesema kujua idadi halisi ya watu itawezesha kutengeneza fursa za kimaisha na kimaendeleo ya wananchi pamoja na serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Takwimu, Jocye Saul, alisema ukusanyaji wa sensa umekuwa shirikishi.
Leave a comment