November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

WHO kutokomeza kipindupindu mwaka 2030

Spread the love

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limeeleza matumaini yake ya kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya kipindupindu duniani sambamba na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 90 ifikapo 2030, anaandika Shaban Matutu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi anayehusika na masuala ya dharura katika shirika hilo Dk. Peter Salama alipokuwa akizungumza na waandishi habari mjini Geneva.

Mkurugenzi huyo amesema shirika hilo lingeweza kuchukua hatua za haraka na kutoa chanjo zaidi ili kupambana na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa kipundupindu nchini Yemen kwa mwaka huu.

Dk. Peter Salama ameeleza matumaini yake kwamba , wanakaribia kufikia ukingoni kuhusiana na ugonjwa huo unaoweza kuzuilika, unaosababishwa na vijidudu vilivyomo katika maji ambao umefikia maambukizi ya watu 700,000 na kusababisha zaidi ya vifo vya watu 2,000 mwaka huu.

Lengo ni moja kati ya malengo makubwa ya shirika la WHO kuutokomeza kabisa ugonjwa huo ama kupunguza kwa kiasi kikubwa ugonjwa huo.

Juhudi kama hizo tayari zipo kwa ugonjwa wa kupooza, malaria, surua, na ukimwi. Hivi sasa, ni ugonjwa wa tetekuwanga ambao umekwisha tokomezwa katika uso wa dunia.

India na nchi zilizoko katika bara la Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara zinakabiliwa na changamoto ya muda mrefu kupambana na kipindupindu.

error: Content is protected !!