WATU 30 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kughushi nyaraka za mafao ili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 9 Aprili 2024 na Kamanda wa Jeshi la Polisi wa kanda hiyo, SACP Jumanne Muliro, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amesema polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kwa kushirikiana na maafisa kutoka NSSF.
Amesema watafikishwa mahakamani kwa makosa ya kujihusisha na mambo ya kughushi nyaraka mbalimbali na kupanga mpango wa kuliibia shirika hilo.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na maofisa kutoka NSSF limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 30, wanaotuhumiwa kughushi nyaraka mbalimbali zinazohusiana na mafao ya mfuko huo kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,” amesema Kamanda Muliro na kuongeza:
“Sehemu ya ushahidi imepatikana na watafikishwa mahakamani kwa kosa la kujihusisha na mambo ya kughushi nyaraka mbalimbali na kupanga mpango wa kuliibia shirika hilo.”
Leave a comment