SERIKALI ya Tanzania imesema, hadi kufikia juzi Ijumaa tarehe 15 Oktoba 2021, takiribani wananchi 940,000 walikuwa wamepata chanjo ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya korona (UVIKO-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Shughuli ya utoaji wa chanjo ilizinduliwa tarehe 28 Julai 2021, Ikulu ya jijini Dar es Salaam na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa yeye mwenyewe kuchanjwa chanjo aina ya Johnson & Jonson.
Leo Jumapilo, tarehe 17 Oktoba 2021, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, akitoa taarifa ya wiki ya utendaji wa Serikali akiwa jijini Mwanza amesema, shughuli ya utoaji wa chanjo inaendelea vizuri.
Amesema, Serikali ya Tanzania ilipokea dozi 158,4000 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), kupitia mpango wake wa kusaidia nchi kupata chanjo.
“Kati ya zile chanjo 158,4000, mpaka sasa Watanzania zaidi kwa takwimu za mpaka juzi zaidi ya 940,000 walikuwa wameshapata chanjo hii. Kwa hivyo kazi inakwenda vizuri,” amesema Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo
Msigwa amesema chanjo za awamu ya pili zilizoingizwa hivi karibuni, aina ya Sinopharm kutoka nchini China, zimeanza kusambazwa katika halmashauri.
“Tumeshaleta chanjo nyingine dozi 165,000 zimeshafika aina ya Sinofarm kutoka China, tunatoa mara mbili, unachoma matra ya kwanza, kisha ukachome ya pili,” amesema Msigwa.
Msigwa amesema mwishoni mwa Oktoba 2021, Serikali inatarajia kupokea dozi nyingine 500,000 za chanjo ya UVIKO-19, aina ya Pfizer.
Pia, amesema kupitia mpango wa Covax Facility wa WHO, Serikali inatarajia kupata chanjo milioni 12.
Leave a comment