December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kilio cha kuunganishiwa umeme na NIDA chaibuka, serikali yajibu

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania, imeombwa kuingilia kati changamoto zinazokwamisha huduma zinazotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamalaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Maombi hayo yametolewa leo Jumapili, tarehe 17 Oktoba 2021, katika mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki ya utendaji wa Serikali, jijini Mwanza.

Kilio cha baadhi ya ofisi za TANESCO kuchelewa kuwaunganishia umeme wananchi, kilitolewa na Mfanyakazi wa Redio Free Africa, Paulina David, aliyehoji msimamo wa Serikali dhidi ya changamoto hiyo.

“Serikali ilisema kuunganshiwa umeme ni Sh.27,000, lakini changamoto iliyopo sasa hivi ni baadhi ya watu wanapoenda kulipia zile gharama, kumekuwa na shida ya kupelekewa umeme,” ameuliza Paulina na kuongeza:

“Je msimamo wa Serikali ni upi? Ni hii Sh.27,000 au kuna gharama nyingine wananchi wanatakiwa watoe? Maana kumekuwa na changamoto mfano kuna watu wamelipa Julai hadi sasa hawajaunganishiwa umeme.”

Akiongezea katika swali hilo, Rais wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakar Kasan, amedai kuna baadhi ya maafisa wa TANESCO wanagoma kuwaunganishia umeme wananchi wanaolipa Sh. 27,000 kwa madai kwamba fedha ni ndogo.

“Nikisaidia swali la Paulina, ni kwamba unapokwenda kulipia hizo Sh.27,000 wafanyakazi wa TANESCO wanasema ile kauli haikuwa ya Serikali, hatuwezi kuweka kwa Sh.27,000 hawawapi umeme sababu wanaigomea kichichini ile 27,000. Wanasema hiyo ni hela kidogo sana,” amesema Kasan.

Akijibu malalamiko hayo, Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ametoa wito kwa wananchi wanaokumbana na kadhia hiyo watoe taarifa ili Serikali iwachukulie hatua wahusika.

“Maelekezo ya Serikali ni kwamba, wananchi waunganishiwe umeme kwa Sh. 27,000, naomba kutoa wito kwa Watanzania kama kutakuwa na mfanyakazi wa TANESCO ambaye anakataa kuunganisha umeme toa taarifa kwa viongozi hatua zitachukuliwa, sababu maelekezo ya Serikali lazima yatekelezwe,” amesema Msigwa.

Hata hivyo, Msigwa amesema changamoto ya TANESCO kuchelewa kuunganishia umeme wananchi inasababishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kuitaka huduma hiyo, baada ya Serikali kushusha gharama zake kutoka Sh. 300,000 hadi Sh.27,000.

Mbali na changamoto ya TANESCO, Kasan aliiomba Serikali itatue changamoto ya uchelewaji wa kutoa vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na NIDA.

“Serikali itueleze ukweli kuhusu kadi za NIDA, nilimsikia vizuri waziri akisema kadi za NIDA zipo kama umejisajili nenda kwenye mkoa wako uliposajiliwa mkachukue. Najitaja mwenyewe nimesajiliwa zaidi ya mwaka mmoja sijapata kadi ya NIDA mpaka leo,” amesema Kasan.

Msigwa amejibu swali hilo akisema, Serikali inalifanyia kazi suala hilo ili kuhakikisha wananchi wanapata vitambulisho hivyo kwa wakati.

“Serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha inaongeza uwezo wa uchapishaji vitambulisho, ili Watanzania wengi wapate vitambulisho kwa haraka zaidi, ni matarajio yetu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tutakuwa tumepunguza tatizo la watu wanaosubiri vitambulisho vya uraia,” amesema Msigwa.

Msigwa amesema, hadi sasa takribani Watanzania milioni 22 wamehakikiwa kwa ajili ya kupata vitambulisho vya NIDA, na kwamba wengi kati yao wamevipata.

Aidha, Msigwa amesema, kuna vitambulisho 1,300,000 havijachukuliwa.

error: Content is protected !!