Wananchi wa kijiji cha Songambele kilichopo kata ya Magamba wilayani Songwe mkoani humo, wameiomba serikali kuharakisha ujenzi wa kituo cha afya Ileza ambacho ujenzi wake haujakamilika kwa miaka nane sasa.
Kituo hicho kilichoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2014, kinategemewa na wakazi 55,000 wa kata tano wanaolazimika kutembea umbali mrefu hadi Mkwajuni kupata huduma za tiba. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe…(endelea).
Wakizungumza leo Jumamosi na MwanaHALISI Online kwa nyakati tofauti wakazi wa eneo hilo la Magamba, wamesema ujenzi huo ulianza mwaka 2014 chini ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya kisha kuhamishiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mkoani Songwe.
Mmoja wa wakazi hao wa Songambele, Adam Mponzi amesema ujenzi wa kituo hicho uliendelezwa mwaka 2018 kwa kumalizia jengo ya huduma za nje (OPD) lililokuwa likijengwa kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2014.
“Tumeona serikali imeleta fedha ya kumalizia majengo mengi lakini bado mengine hayajakamilika licha ya huduma za nje zimeanza kutolewa lakini tunaomba majengo yakamilishwe tuepuke kutembea kilometa 72 kwenda wilayani kutibiwa,’’ amesema Mponzi.
Diwani wa kata hiyo, Kapala Makelele amesema kituo hicho kwa sasa kinategemewa na wakazi 55,000 wa kata 5 kwani mto Mtua ukijaa wananchi hawawezi kwenda upande wa pili kutibiwa.
Amesema amekaa kwenye nafasi ya udiwani tangu mwaka 1984 wakiwa chini ya wilaya ya Chunya na amedumu vipindi 8 hivyo anafahamu mazingira mabovu ya kata hizo hivyo ni vema mradi huo ukamaliziwa ili kuwapunguzia wananchi adha ya kupata matibabu.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga mkuu, Mratibu wa afya uzazi na mtoto Dk. Lydia Kyumana amesema wananchi walianzisha ujenzi huo kwa thamani ya Sh 80 milioni kisha serikali ikatoa Sh 542 milioni ambazo zimewesha ujenzi wa mradi huo kufikia asilimia 98 huku huduma za nje (OPD) zianza kutolewa.
Aidha, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Cecilia Kavishe amesema kupitia mapato yao ya ndani wanatarajia kupeleka Sh. 135 milioni ili kukamilisha majengo yote yaliyosalia kwani dawa na vifaa tiba vimekwishapelekwa.
Leave a comment