WANAFUNZI kutoka mikoa mbalimbali nchini walioanza masomo ya kidato cha tano katika shule mpya ya wasichana Dk. Samia -SSH iliyopo kijiji cha Namole Halmashauri ya mji Tunduma mkoani Songwe, wameiomba serikali kuwajengea uzio utakaowawezesha kuongeza umakini kwenye masomo na kuepuka vishawishi. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe…(endelea).
Shule hiyo iliyofunguliwa tarehe 8 Oktoba mwaka huu, ilijengwa na Serikali kwa thamani ya Sh bilioni tatu kati ya hizo, Sh bilioni moja zikitolewa na halmashauri ya mji Tunduma kupitia mapato yake ya ndani.
Wakizungumza leo Alhamis na MwanaHALISI Online baadhi ya wanafunzi waliojiunga na shule hiyo, mbali na kuipongeza serikali kwa ujenzi wa shule hiyo, wameiomba Serikali na wadau wa elimu kujenga uzio na kununua jenereta pindi umeme utakapokatika.

Pendo Mwalwiba kutoka mkoa wa Songwe, anayesoma mchepuo wa HKL amesema amesema iwapo uzio huo ukijengwa, utawaepusha na vishawishi na kusoma kwa uhuru.
Ombi hilo la Pendo liliungwa mkono na Jenifer Simon anayetoka jijini Mwanza. Jenipher ambaye amechukua mchepuo wa HGE, amesema ndoto yake kuwa mwalimu ili aweze kuelimisha jamii.
Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Bedon Mwaswala amesema shule hiyo iliyoanza kwa kupokea wanafunzi 192 wa kidato cha tano, mwakani wanatakiwa kuwa na wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Amesema uwepo wa shule hiyo kutainua ufaulu kwa wasichana hasa wa shule hiyo kutokana na usalama uliopo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji Tunduma, Philimon Magesa amesema shule hiyo ni moja ya shule nne za kimkakati nchini kwa mkoa wa Songwe ambayo imejengwa Tunduma.
Amesema kazi kubwa iliyopo ni ukamilishaji wa majengo yaliyobaki ikiwemo uzio na jenereta la umeme, kwani hoja za wanafunzi hao zina mashiko.
Leave a comment