MHASIBU wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula ya alizeti – Malaika Sunflower Oil, Ester Lumambo amewashauri wakulima wa mazao ya alizeti nchini kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kulima kilimo chenye tija badala ya kulima mazao ya kujikimu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma (endelea).
Lumambo ametoa ushauri huo umetolewa leo tarehe mosi Agosti 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi yanayofanyika kwa mikoa miwili ya Dodoma na Singida katika viwanja vya maonesho Nzuguni Jijini Dodoma.
Amesema wakulima wanatakiwa kulima kilimo ambacho kitawapatia manufaa ya kuingia kwenye soko kwa urahisi na kujipatia kipato kizuri na kuwafanya wanunuzi kununua bidhaa ambazo ni bora na zenye uhakika.
“Sisi ni wafanyabiashara ambao tunanunua mazao ya alizeti kwa wakulima, lakini kuna changamoto ambazo tunakutana nazo kutoka kwa baadhi ya wakulima na changamoto kubwa ni wakulima wanakuwa na mbegu ambazo hazina mafuta mengi.
“Na tatizo hilo linatokana na kukosekana kwa utaalamu mzuri wa kujua ni mbegu gani mkulima anatakiwa kupanda ili waweze kupata mazao mengi na ambayo hayana changamoto yoyote kwenye soko” ameeleza mhasibu huyo.
Aidha, Mhasibu huyo amewahimiza kujenga tabia ya kununua bidhaa ambazo zipo kwenye kiwango cha ubora kwa nia ya kulinda na kutunza afya zao.
Naye mmoja wa washiriki wa maonesho hayo ambaye ni mkulima, kutoka wilaya ya Mpwapwa aliyejitamulisha kwa jina la Levison Lemanya amesema kuwa maonesho hayo yatalenga zaidi kuwaelimisha wakulima ili kulima kilimo chenye tija.
Leave a comment